Tuesday, 4 October 2016

#YALIYOJIRI>>>>Rais Kabila Wa Congo-DRC Aweka Jiwe La Msingi Bandarini Jijini Dar Es Salaam .Kasema Nchi Yake Itaendelea Kutumia Bandari Yetu Kupitisha Mizigo.Fahamu zaidi hapa.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila Kabange ameweka jiwe la msingi la jengo la Kituo cha Pamoja cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ambalo limejengwa kwa lengo la kuwaweka pamoja wadau wote wanaotoa huduma katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni juhudi za kuboresha huduma na kupunguza gharama kwa watumiaji wa bandari hiyo.

Hafla ya uwekaji jiwe la msingi la jengo hilo refu kuliko yote Afrika Mashariki na kati imefanyika leo tarehe 04 Oktoba, 2016 na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Akizungumza kabla ya kuwekwa jiwe hilo la msingi Rais Magufuli ameishukuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwa mteja mkubwa wa bandari ya Dar es Salaam na amesema aliamua jiwe la msingi la jengo hilo liwekwe na Rais wa Kongo kwa kutambua umuhimu wa nchi yake katika biashara ya bandari ya Dar es Salaam na pia undugu na urafiki wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizi mbili.

Rais Magufuli amemhakikishia Rais Kabila kuwa kama ambavyo Serikali yake imechukua hatua kadhaa za kurekebisha kasoro zilizokuwepo katika bandari hiyo, itaendelea kujenga mazingira mazuri zaidi kwa wafanyabiashara wa Kongo kutumia bandari hiyo ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa, kuongeza muda wa kutunza mizigo inayoshushwa kutoka siku 14 hadi siku 30, kuanzisha bandari kavu katika eneo la Ruvu mkoani Pwani na kuinua ari ya wafanyakazi wa bandari kutoa huduma bora.

"Mhe. Rais Kabila bandari yetu ilifikia mahali pa kuandika rekodi ya kupotea kwa meli kwenye taarifa za bandari, kuna wakati hapa zilipotea meli 60, lakini pia mizigo ya watu ilikuwa inapotea na wafanyabiashara walikuwa wanaombwa rushwa.

"Kuna baadhi ya wafanyakazi wa bandari waliifanya hii bandari kama mali yao, walikuwa wanaondoka na fedha za rushwa kwenye buti za magari, naomba nikuhakikishie kuwa haya hayatatokea tena, na yakitokea Mhe. Balozi wa Kongo upo hapa njoo unieleze mimi au mwambie Makamu wa Rais au Waziri Mkuu" amesisitiza Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli pia amempongeza Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha ujenzi wa jengo hilo la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania na kwamba anaamini litasaidia kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Kongo na nchi nyingine zinazotumia bandari ya Dar es Salaam.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila Kabange amemshukuru Rais Magufuli kwa heshimu kubwa aliyompa yeye na nchi ya Kongo ya kuweka jiwe la msingi la jengo hilo na amesema kutokana na Tanzania kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha huduma za bandari ya Dar es Salaam mizigo ya Kongo itapitia bandari hiyo.

"Mhe. Rais Magufuli bandari hii ipo Dar es Salaam lakini bandari hii ni ya kwetu sote, mashariki ya Kongo inapakana na nchi nne za Tanzania, Rwanda, Burundi na Uganda lakini asilimia 50 ya mizigo inatoka Tanzania hususani katika bandari ya Dar es Salaam.

"Nimefurahi pia kuwa katika juhudi za Tanzania kuboresha bandari pia mnaboresha barabara na bandari ndogo ndogo za ziwa Tanganyika, hili ni jambo muhimu kwa sababu sasa mizigo ya Kongo itasafiri kwa urahisi na wafanyabishara wa Kongo waliokuwa wameacha kutumia bandari ya Dar es Salaam watarudi" amesema Rais Kabila.

Mhe. Joseph Kabila Kabange amesema katika miaka ya 70 na 80 Kongo ilikuwa ikizalisha shaba kiasi cha tani laki 1 lakini hivi sasa inazalisha hadi tani Milioni 1.2 na zote hizi zinategemewa kusafirishwa nje ya nchi kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kununua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 na ameunga mkono mpango wa kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na Kongo huku akibainisha kuwa nchi yake pia itanunua ndege kwa ajili ya kuimarisha zaidi usafiri wa anga kati ya nchi hizi mbili.

Mapema kabla ya Marais wote wawili kuzungumza, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deodatus Kakoko alisema jengo hilo lina ghorofa 35, urefu wa meta 157, ukubwa wa meta za mraba 65,115 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika tarehe 31 Desemba, 2016 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 130.

Rais Kabila ambaye aliingia hapa nchini jana tarehe 03 Oktoba, 2016 kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu, jioni ya leo atahudhuria dhifa ya kitaifa katika ukumbi wa Ikulu Jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa kwa ajili yake na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

04 Oktoba, 2016

0 comments:

Post a Comment