Saturday, 4 June 2016

#YALIYOJIRI>>>Mambo Mawili Yanayoibana Serikali Katika Mgogoro wa Wanafunzi 7000 Waliotimuliwa UDOM.Fahamu zaidi hapa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitilla Mkumbo amesema kuna mambo mawili yanayoibana Serikali katika mgogoro wa wanafunzi waliotimuliwa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Akizungumza jana kwenye kipindi cha ‘Kipima Joto’ kinachorushwa na kituo cha luninga cha ITV, Profesa Mkumbo alisema Serikali haiwezi kukwepa lawama, kwa sababu ndiyo iliyoanzisha utaratibu wa kudahili wanafunzi wa kidato cha nne kupitia mfumo maalumu kabla ya kuanza kusoma shahada ya chuo kikuu.

Pia, alisema Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), haiwezi kuhusika moja kwa moja kwenye udhaifu uliojitokeza katika udahili wa wanafunzi hao, bali Seneti ya Udom inapaswa kuwajibika katika hilo.

Alisema kuna udhaifu wa kiutendaji kwa seneti hiyo yenye mamlaka ya kudahili wanafunzi wenye sifa ambayo iliiacha kazi hiyo  mikononi mwa TCU.

Mkumbo alisema kazi ya TCU ni kuidhinisha majina ya wanafunzi waliokwisha dahiliwa na chuo husika na si kuchagua.

“Chuo chochote ndicho kinachagua wanafunzi wenye sifa wanazozihitaji, inashangaza kuona Udom imefanyiwa kazi hiyo, baraza na seneti wanapaswa  kuwajibika kwanza, TCU haiwezi kukichagulia chuo wanafunzi,” alisema Profesa Mkumbo.

Hata hivyo, alitoa angalizo kwa Serikali kutodharau mfumo huo wa udahili kwa wanafunzi ambao hawakuhitimu Kidato cha Sita kama ilivyoamriwa na Serikali ya Awamu ya Nne, kuwa upo na unatumika duniani kote.

“Ila kama Rais (John) Magufuli hautaki na ameona turudi kwenye mfumo wa zamani ambao mwanafunzi anapaswa kufaulu  kidato cha sita ndiyo ajiunge na chuo kikuu sawa,  lakini atambue kuwa kuna hasara na faida zake, vyuo vingi vinaweza kufungwa,” alisema Mkumbo

Mbali ya mfumo huo, profesa huyo alisema upo mfumo mwingine wa udahili kwa mtu yeyote mwenye umahili katika taaluma yake kusoma shahada kwa kuzingatia vigezo maalumu vilivyowekwa.

“Ila hakuna jinsi, nadhani  TCU wamemsikia Rais kuwa hataki njia za mkato tena.”

Mei 29, Udom iliwasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya ualimu wa sayansi kwa ngazi ya stashahada na kuwataka waondoke chuoni mara moja.

Amri hiyo iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, ilisema Serikali imeamua warejee kwao na wataelezwa mustakabali wao mapema iwezekanavyo.

Hata hivyo, Rais John Magufuli juzi alisema baadhi yao walikuwa vilaza, hivyo wajitafutie mahali pa kwenda huku wenye ufaulu wa daraja la kwanza na pili aliahaidi kuwa wataandaliwa utaratibu.

0 comments:

Post a Comment