BAADA ya juzikati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa hati ya kukamatwa kwa meneja wa Mbongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ (picha kubwa) kwa kutotii amri ya mahakama iliyomtaka kumlipa Shehe Hamis Mbonde Sh. Milioni 250 kwa kupatikana na hatia ya kumtapeli kazi zake za mawaidha, meneja huyo alijikuta akirudishwa kortini hapo huku akihenyeshwa.
Kesi hiyo ambayo ilisikilizwa kwa zaidi ya miaka miwili na kutolewa hukumu, Februari, mwaka huu ilionesha kuwa, Kampuni ya Tip Top Connection ambayo Babu Tale ni mmoja wa wamiliki, ilitoa na kusambaza kwa kuuza DVDs za mawaidha ya Shehe Mbonde (mojawapo Uzito wa Kifo) bila makubaliano maalum.
Kwa mujibu wa chanzo, Babu Tale alifikishwa mahakamani hapo, Jumanne iliyopita chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi huku akionekana kuchoka sana, pengine kwa mawazo au kwa kutolala sawasawa kama binadamu.
Mbali na hali hiyo, pia Babu Tale siku hiyo alivaa suruali ya jinZi iliyochanika kwenye magoti. Haikujulikana ni fasheni au kulikuwa na misukosuko alikotokea. Chini, kwa maana ya miguuni alivaa ndala au kandambili hali iliyompotezea uhalisia wake.
Afande mmoja aliyekuwa kwenye msafara wa gari lililombeba Babu Tale, aliliambia Amani kuwa, jamaa huyo alitokea Mahabusu ya Kituo cha Polisi, Mbezi Kwa Yusuf jijini Dar ambako alilala kwa siku moja baada ya kukamatwa, Jumatatu jioni, nyumbani kwake, Mbezi ya Kimara.
Hata hivyo, mahakamani hapo, Babu Tale alikuwa na mawakili wanne kwa ajili ya kutengua hukumu ya awali ya mahakama kuhusu kutakiwa kulipa kiasi hicho cha pesa, lakini baada ya shauri hilo kusikilizwa kwa zaidi ya dakika 45, ilishindikana.
Mawakili wake wakaomba muda wa kwenda kupitia tena shauri zima mwanzo hadi mwisho jambo lililomsukuma hakimu kuahirisha kesi hiyo mpaka Ijumaa (kesho).
Ilizungumzwa mahakamani hapo kuwa, Babu Tale aliachiwa huru kwa masharti ya kufika mwenyewe Ijumaa bila kukosa.
Gazeti hili lilimtafuta Babu Tale bila mafanikio yoyote kwani simu yake ya mkononi haikupatikana hewani baada ya kutoka mahakamani.
Kesi ya msingi ya Babu Tale ilishasikilizwa na hukumu kutolewa ambapo alitakiwa kulipa fidia hiyo kwa mlalamikaji lakini ikadaiwa kuwa, meneja huyo hakutii hukumu hiyo.
0 comments:
Post a Comment