Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) limemteua Sebastian Nkoma kuwa Kocha Mkuu wa
timu ya soka taifa ya wanawake wa Tanzania Bara maarufu kwa jina la
Kilimanjaro Queens ambayo kwa mara ya kwanza inakwenda kushiriki
mashindano ya kuwania Kombe la Afrika Mashariki na Kati yatakayofanyika
kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, 2016 jijini Jinja, Uganda.
Uteuzi huo wa Nkoma unakwenda
sambamba na wasaidizi wake, ambao ni Hilda Masanche na Edna Lema wakati
Meneja wa timu hiyo, Furaha Francis. Mtunza vifaa ni Esther Chabruma
maarufu kwa jina la Lunyamila.
Kabla
ya uteuzi huo, Nkoma alikuwa Kocha Msaidizi wa timu ya Mpira wa Miguu
ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ambayo kwa
sasa ipo kambi ndogo ya kwenye hosteli za TFF kujiandaa na kambi kubwa
itakayofanyika Shelisheli kabla ya kuivaa Congo – Brazzaville kwenye
mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika kwa vijana wenye umri huo.
Fainali hizo zitapigwa Aprili mwakani, nchini Madagascar.
Kilimanjaro
Queens inatarajiwa kuanza mazoezi ya leo, Septemba mosi, 2016 ambako
wachezaji watakuwa wanakwenda mazoezini Uwanja wa Karume, Ilala na
kurudi nyumbani hadi Jumapili ambako Jumatatu itasafiri kwenda Uganda
kupitia Bukoba mkoani Kagera itakakoweka kambi tena ya siku nne.
Septemba
8, mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi ambayo pia
itakuwa njiani kwenda Uganda kwenye mashindano hayo yanayoratibiwa na
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Kwa
mujibu wa CECAFA, michuano hiyo itafanyika jijini Jinja na Tanzania
ambayo inaongoza kwa ubora wa viwango vya Mpira wa Miguu kwa nchi za
Afrika Mashariki imepangwa kundi B ikiwa pamoja na timu za Rwanda na
Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi, Zanzibar
pamoja na mwenyeji Uganda.
Tanzania
itafungua michezo hiyo kwa kucheza na Rwanda Septemba 12, 2016 kabla ya
kucheza na Ethiopia Septemba 16, 2016. Rwanda na Ethiopia zitacheza
Septemba 14, 2016 wakati kundi A Zanzibar itakata utepe kwa kucheza na
Burundi na siku hiyohiyo, Uganda itacheza na Kenya.
Michezo
mingine ya kundi A itakuwa ni kati ya Burundi na Kenya zitakazocheza
Septemba 13, 2016 ambako siku hiyohiyo Zanzibar itacheza na Uganda.
Septemba 15, Kenya itacheza na Zanzibar na Uganda itafunga hatua ya
makundi kwa siku hiyo kwa kucheza na Burundi.
Nusu
fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika Septemba 20,
2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na nne.
Mashindano
ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya kwanza jambo
linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake
kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania inatarajiwa kuanza
kambi Septemba mwanzoni kwa mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani kwa
wiki moja na baadaye wataingia kambini moja kwa moja tayari kwa safari
ya Uganda.
0 comments:
Post a Comment