Kichanga chenye umri usiozidi wiki moja ambacho hakikufahamika jina
lake, kilitelekezwa katika nyumba ya kulala wageni inayojulikana kwa
jina la Kibara, iliyopo Musoma Mjini Ijumaa iliyopita, Risasi
Mchanganyiko lina mkasa mzima.
Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa Ustawi wa Jamii katika Hospitali ya Mkoa wa
Musoma, aliyejulikana kwa jina moja Clavery, kichanga hicho
kilitelekezwa na mama yake mzazi, aliyefika katika gesti hiyo akiwa na
watoto wake wawili, mmoja mkubwa akiwa na umri unaokadiriwa kuwa miaka
miwili.
Alisema alipopanga katika nyumba hiyo, alikaa kwa muda kabla ya kumuomba
mhudumu wa nyumba hiyo, amuangalizie mtoto wake huyo, wakati yeye
akienda kutafuta chakula kwa ajili ya mtoto mkubwa, mfanyakazi huyo
hakuwa na kipingamizi.
“Sasa akiwa anaendelea na shughuli zake, mara akasikia mtoto huyo
mchanga analia, akajua ni jambo la kawaida na mzazi wake atarudi mapema,
lakini muda ukazidi kwenda na hakutokea, akalazimika kuwaita akina mama
majirani ndipo waliamua kwenda kutoa taarifa polisi,” alisema ofisa
huyo.
“Akina mama hao waliokuwa wakimgombea ili kumtazama mtoto, hawakuamini
kama mama anaweza kumtelekeza mtoto wake wa kumzaa, wakamchunguza kama
ana ulemavu wowote, lakini wakamkuta mzima, ndipo wakampeleka polisi,”
alisema.
Baada ya kufika kituo cha polisi na kutoa taarifa hizo, askari hao
walimpeleka mtoto huyo hospitalini, ambako alipokelewa na kuanza
kuangaliwa tangu siku hiyo hadi leo na mama yake hajulikani alipo.
“Alipoletwa hapa alikuwa katika hali mbaya, tumejaribu kumhudumia kwa
kadiri tunavyoweza na hali yake inaendelea vizuri, hii siyo mara ya
kwanza kukutana na kesi kama hizi, mwaka jana kuna mwingine aliletwa
hapa naye akitorokwa na mama yake, hatukuwa tukilijua jina lake,
tukaamua kumuita Eliah.
“Sasa na huyu naye ameletwa na jina lake hatulijui, kwa hiyo sisi hapa
tumeamua kumwita jina la Elisha, kwa kuwa ni wa kiume, tutaendelea kuwa
naye hadi hapo baadaye uamuzi mwingine utakapochukuliwa na serikali,”
alisema Clavery, aliyedai kukaimu nafasi ya ofisa ustawi katika
hospitali hiyo.
Jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhan Ng’azi
hazikuzaa matunda kwani simu yake ya kiganjani haikupokelewa kila
ilipopigwa.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment