Hatimaye kamati maalum iliyoundwa na waziri wa habari, utamaduni, sanaa
na michezo, Nape Nnauye kuhusu tukio la mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda kuzivamilia studio za Clouds Media Group, Ijumaa iliyopita
akiwa na askari wenye silaha nzito, imekabidhi ripoti yake.
Kamati hiyo iliyoundwa na watu mbalimbali akiwemo mhariri mtendaji wa
New Habari Corporation, Deodatus Balile, imethibitisha kuwa ni kweli
Makonda alienda katika kituo hicho usiku wa Ijumaa akiwa na askari na
kuwashinikiza watangazaji wa kipindi cha Da W’keend Chat show
(Shilawadu) warushe kile alichokiita kipindi chake na baada ya kugoma
aliwatishia mambo kadhaa.
Kamati hiyo imesema moja ya vitisho hivyo ni kuwakagua watangazaji hao
kama wanahusika na uuzaji wa madawa ya kulevya ‘ama kuwabana wadhamini
wa kipindi hicho na pengine kuwaingiza kwenye orodha ya kuuza dawa za
kulevya.’
Imedai kuwa watangazaji wa kipindi hicho walipatwa na taharuki kubwa
kiasi cha kujikuta wakilia na kushindwa kufunga kipindi chao. Imesema
mkuu huyo wa mkoa alitumia takriban saa nzima katika kituo hicho na
kuwataka wafanyakazi wake kuwa yaliyotokea yabaki ndani ya siku hizo.
Kamati hiyo imesema tukio hilo limeingilia uhuru wa uhariri na uvunjifu
wa amani kutokana na vitisho alivyovitoa mkuu huyo wa mkoa. Pia kamati
imekiri kuwa Makonda alikuwa ‘mgeni mwenyeji’ kwenye kituo hicho na
March 14 alikaaa katika ofisi hizo hadi saa 10 alfajiri kuhariri na
watayarishaji kipindi maalum cha kuadhimisha mwaka mmoja wa uongozi
wake.
Hata hivyo wafanyakazi wa kituo hicho wamedai kuwa mkuu huyo wa mkoa
hakuwahi kwenda na askari wenye silaha katika siku zingine kabla ya
March 17. Pia imedai kuwa hakuna mtangazaji aliyepigwa wala kuumizwa
kwenye tukio hilo.
Mapendekezo ya kamati hiyo ni:
1. Mkuu wa mkoa aombe radhi Clouds na kwa wanahabari wote
2. Waziri husika atoe taarifa kwa mamlaka husika ili Mkuu wa Mkoa achukuliwe hatua
3. Vyombo vya usalama kufanya uchunguzi juu ya askari kuingia Clouds na silaha za moto
4. Kampuni ya Clouds ipitie upya kanuni, miongoni na sheria za
utangazaji ili kuwa na udhibidi wa watu kuzoea kuingia mara kwa mara
pasipo kuwa na taaluma ya habari
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment