Kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa ya mfumo wa mkojo (UTI) na uzazi
kwa wanawake, hii inasababishwa na sababu nyingi ikiwemo ya kukosa
uelewa sahihi wa kanuni za afya na usafi wa mwili pamoja na mazingira
yanayomzunguka mwanamke.
Mada za usafi wa mwanamke ni pana sana siwezi kumaliza kusema kila kitu,
hivyo leo nitajikita zaidi katika matumizi sahihi ya pedi na mambo ya
kuzingatia kabla ya kunua pedi. Wadada wengi wamekuwa wakitumia pedi na
kuziacha zikizagaa mitaani hali inayofanya nijiulize kama tu ameshindwa
kujua sehemu sahihi ya kuhifahi au kutupa pedi aliyotumia yeye
mwenyewe,
Je anauelewa upi katika matumizi sahihi ya pedi hizo kabla hajazitumia?
Somo la leo nitajikita katika njia sahihi ya kuchagua na kutumia pedi,
makosa yanayofanywa katika matumizi ya pedi na ushauri juu ya matumizi
sahihi ya pedi na vitambaa kwa wale wanaovitumia.
Yafuatayo ni makosa yanayofanywa katika uchaguzi na matumizi ya pedi kwa wanawake:
1. Kutonawa mikono kabla na baada ya kutumia pedi. Mikono hushika sehemu
mbalimbali hivyo kuna uwezekano ikawa na vimelea vinavyosababisha
magonjwa kwa hiyo kushika pedi bila kunawa mikono kwa sabuni kunaweza
kuhamisha vimelea hivyo kutoka mikononi na kwenda kwenye pedi
inayotegemewa kuvaliwa.
2. Kutunza pedi bafuni au chuoni. Wadada wengi hupendelea kutunza pedi
zao chooni/bafuni. Vyumba vingi vya choo/bafu havina mwanga wa kutosha
na kuwa na unyevunyevu hali inayoweka mazingira mazuri ya ukuaji wa
vimelea vya magonjwa kama bacteria na kitendo cha kutunza pedi katika
sehemu hizo kunaweza kusababisha kuhama kwa vimelea hao kutoka
bafuni/chuoni kwenda kwenye pedi isiyovaliwa na kupelekea pedi hizo kuwa
na vimelea vya magonjwa na mwanamke anakuwa katika hatari za kupata
maambukizi.
3. Kutoangalia muda wa matumizi wa pedi kabla ya kutumia au baada ya
kuzihifadhi kwa muda mrefu hali inayopunguza kiwango cha ufanisi cha
pedi sababu ya kuisha kwa muda wake wa matumizi.
4. Kununua pedi zinazouzwa kiholela kwa njia ya utangazaji na za bei
rahisi (promotion) ambazo baadhi zimeonekana kutengenezwa kwa malighafi
zilizo chini ya kiwango au kukaa kwa muda mrefu hivyo kuuzwa kwa bei
rahisi ili zitoke na kutumika haraka kabla ya kuisha muda wake.
5. Kutumia pedi ambazo zipo katika majaribio maalum. Kama tunavyojua
kuna kila aina za pedi mpya katika soko kwa kadri siku zinavyozidi
kwenda na baadhi ya pedi huingizwa sokoni kinyemela pasipo tafiti za
kutosha na bila hata kuthibishwa na mamlaka husika.
6. Kutumia pedi kwa muda mrefu. Wanawake wengi hususani katika nchi
zinazoendelea huwa hawamudu kutumia pedi moja kwa muda wa masaa mawili
kama inavyoshauriwa na wataalamu hivyo kujikuta katika hatari ya kupata
magonjwa ya mfumo wa mkujo na njia za uzazi .
7. Kupendelea pedi zenye uwezo mkubwa wa kufyonza unyevunyevu ili
ivaliwe muda mrefu pia ni tatizo sababu kwa kadri muda wa kuvaa pedi
moja unapozidi kuongezeka na hatari za maambukizi ya magonjwa pia
inazidi kuongozeka.
Wanawake wanashauriwa kufanya yafuatayo ili kuhakikisha usalama wa afya zao :
1. Kunawa mikono vizuri kwa sabuni kabla ya kugusa pedi ambayo unatarajia kuivaa na baada ya kuvaa kunawa tena mikono vizuri.
2. Kutohifadhi pedi bafuni au chuoni au sehemu yote yenye unyevunyevu na
isiyo na mwanga wa kutosha ili kutotengeneza mazingira ya kukua kwa
vimelea vya magonjwa ndani ya pedi.
3. Kuangalia kwa makini muda wa matumizi ya pedi kabla ya kununua au
baada ya kutunza pedi kwa muda muda mrefu ili kuepuka kutumia pedi
zilizopita muda wake wa matumizi.
4. Kuepuka kununua pedi zinazouzwa kiholela na zisizothibitishwa na TBS
na mamlaka nyingine zenye dhamana ya kuangalia ubora wa pedi hizo.
Mwanamke anatakiwa kuangalia nembo ya uthibitisho wa mamlaka hizo na
kujiridhisha kuhusiana na usalama wa pedi hizo kabla hajanunua.
5. Kubadilisha pedi kila baada ya masaa mawili, kama tunavyojua damu ni
moja wapo ya chakula kizuri sana kwa vimelea vya magonjwa kama bacteria
,unyevunyevu unaosababishwa na kuvaa pedi kwa muda mrefu pia unapelekea
ustawi wa bacteria hao na joto ambalo lipo katika maumbile ya ndani ya
mwanamke vikiungana kwa pamoja vinatengeneza mazingira mazuri ya ukuaji
wa bacteria , hivyo wanawake wanashauriwa kutovaa pedi hizo kwa muda
usiozidi masaa mawili ili kuepuka mazingira hayo.
6. Kuchagua aina sahihi inayokutosha ina kuepuka pedi zinazobana sana
kupita kiwango sababu zinaweza pia kukufanya usiwe huru na kutengeneza
joto la ziada na michubuko katika maumbile ya mwanamke,hivyo mwanadada
unashauriwa kutumia pedi itakayokukaa vizuri(isilegee sana wala kuachia
sana)
7. Kwa wadada wanaotumia vitambaa badala ya pedi ni muhimu pia
kuzingatia kanuni za kiafya na usafi kabla na baada ya kutumia vitambaa
hivyo kama vile kuchagua kitambaa angavu ,kukiloweka na kukifua vizuri,
kuanika kwenye sehemu yenye mwanga wa jua wa kutosha na upepo wa kutosha
pasipo na unyevunyevu ,kupiga pasi kabla ujakihifadhi na kabla ya
kutumia ili kuuwa vimelea vya magonjwa na kuvitunza sehemu nzuri ambayo
haina unyevunyevu, penye hewa na mwanga wa kutosha na mwisho ni
kubadilisha kitambaa hicho kila baada ya masaa mawili pamoja na kunawa
mikono vizuri kabla na baada ya matumizi ya vitambaa hivyo.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment