Jeshi
la Polisi katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, jana liliwapiga
mabomu ya machozi wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bariadi waliokuwa
wakiandamana kupinga Mkuu wa Shule yao, Deus Toga, kuhamishwa.
Wakati wa maandamano hayo yaliyofanyika saa 6.00 mchana wanafunzi hao wapatao 600, walifunga barabara kuu ya Bariadi – Lamadi.
Pia, shughuli mbalimbali za jamii mjini Bariadi zilisimama kwa zaidi ya saa mbili kwa kuwa hakukuwa na utulivu.
Taarifa
zilizopatikana zinasema wanafunzi hao waliandamana wakipinga Mwalimu
Toga kuhamishiwa katika Shule ya Sekondari Giriku.
Kabla
ya wanafunzi hao hawajapigwa mabomu hayo, walianza kuandamana kuelekea
ofisi ya Mkuregenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Merkzedek
Humbe, ambaye ndiye aliyemhamisha Mwalimu Toga.
Wakati
wakielekea ofisini kwa mkurugenzi huyo, askari wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU), waliwadhibiti kabla hawajafika walikokuwa wakielekea.
Taarifa
zinasema walipozuiwa kuelekea ofisini kwa mkurugenzi, walibadili
mwelekeo na kuelekea ofisini kwa mkuu wa Mkoa wa Simiyu ili wakapeleke
malalamiko yao.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, wanafunzi hao walisambaratishwa na askari hao
baada ya kufika jirani na Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu iliyoko
Somanda.
Kutokana
na hali hiyo, wanafunzi hao wa kidato cha kwanza hadi cha sita,
walilazimika kutanda katikati ya barabara ya Bariadi – Lamadi.
Wakiwa
barabarani hapo, walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kutomtaka Mkuu
mpya wa Shule yao, Paul Lutema, aliyepelekwa kushika nafasi ya Mwalimu
Toga.
Pamoja
na nyimbo hizo, walikuwa pia wamebeba mabango mbalimbali yenye ujumbe
tofauti yakiwamo yaliyosema ‘mlimleta kuinua elimu shuleni kwetu
mnamuondoa’, ‘D.E. O’ ni jipu na mengine yalisomeka ‘tunamtaka mkuu wetu
Toga’.
Baada
ya kukaa kwa muda barabarani hapo, walianza kuwarushia mawe polisi
waliokuwa wamewazunguka wasielekee ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Simiyu.
Polisi hao walipozidi kupigwa mawe, walilazimika kujibu mapigo kwa kuwarushia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi hao.
Akizungumza
kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaka jina lake
litajwe , alisema walifikia uamuzi huo baada ya kutangaziwa na mwalimu
wao wa zamu kwamba Mwalimu Toga, alikuwa amehamishwa.
“Baada
ya kutangaziwa hivyo, tuligoma kuingia madarasani na kuamua kuandamana
kwenda ofisini kwa mkurugenzi na ofisi ya mkuu wa mkoa kutaka mwalimu
wetu arudishwe kwa sababu ni mchapa kazi.
“Wanafunzi
wanamtaka Mwalimu Toga kwa sababu tangu afike shuleni kwetu, ufaulu
umeongezeka na migogoro ya shule iliyokuwapo imekwisha.
“Hata
duka la shule lililokuwa limefungwa kutokana na migogoro ya walimu,
limefunguliwa, ndiyo maana wanafunzi wanamtaka mwalimu huyo,” alisema mwanafunzi huyo.
Kutokana
na hali ilivyokuwa, Kaimu Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Festo Kiswaga na Ofisa Elimu wa Mkoa, Julius Nestory, walifika
shuleni hapo kuwatuliza wanafunzi kwa kuzungumza nao.
“Kaimu
mkuu wa mkoa aliwasihi wanafunzi warejee madarasani kuendelea na masomo
kwa kuwa madai yao ya kumtaka Mwalimu Toga yalikuwa yamekubaliwa.
“Lakini
ofisa elimu alisema ofisi ya mkurugenzi ilimhamisha Mwalimu Toga kwa
makosa kwa sababu haikuzingatia sheria na taratibu za uhamisho kwa
sababu mwenye mamlaka ya kuwahamisha wakuu wa shule ni Katibu Tawala wa
Mkoa.
“Ofisi
ya katibu tawala wa mkoa na ofisi yangu ya elimu, hatukuwa na taarifa
za uhamisho huu. Kwa hiyo, tumeamua kuutengua na tunawataka viongozi
wenzangu wasifanye uamuzi bila kufuata utaratibu na sheria,”alisema ofisa elimu huyo.
Mwalimu
Toga alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alikataa kusema chochote
ingawa alionyesha kushangazwa na uamuzi huo wa wanafunzi.
“Naomba
nisizungumze lolote kwa sababu hata mimi nashangaa kusikia haya. Yaani
sielewi ni nini kimesababisha yote haya mpaka wanafunzi kufikia uamuzi
huu, niacheni,” alisema Mwalimu Toga.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment