Tuesday 21 June 2016

Kadi 6 za njano zaiumiza kichwa Yanga.Fahamu zaidi hapa.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema kuwa kadi sita za njano ambazo wachezaji wake wamepata katika mechi ya juzi dhidi ya Mouloudia Bejaia (Mo Bejaia) ya Algeria, zitawaweka kwenye mazingira magumu ya mechi zinazofuata za mashindano hayo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mechi hiyo ya kwanza ya Kundi A, Yanga ililala bao 1-0 wakati TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikipata ushindi mnono wa magoli 3-1 dhidi ya Medeama ya Ghana na kuongoza kwenye kundi hilo.

Wachezaji wa Yanga waliopata kadi katika mechi hiyo ni Mwinyi Haji ambaye ameonyeshwa kadi nyekundu na hivyo kukosa mchezo unaofuata wakati walioonyeshwa kadi za njano ni pamoja na Donald Ngoma, Simon Msuva, Haruna Niyonzima na Amissi Tambwe.

Akizungumza baada ya mechi hiyo iliyofanyika usiku wa kuamkia jana mjini Algiers, Pluijm alisema kwamba kadi hizo zitawafanya wachezaji wake wacheze kwa hofu pale watakapoikaribisha TP Mazembe Juni 28 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Pluijm alisikitika pia kupoteza mechi hiyo licha ya kuwaandaa vizuri wachezaji wake na kuwapa mbinu mbalimbali za kuwakabili Waarabu hao wa Algeria.

Mdachi huyo pia aliwalaumu waamuzi waliochezesha mechi hiyo kutoka Morocco kwa kuwapendelea zaidi wenyeji.

Naye Kocha Msaidizi Juma Mwambusi alisema kuwa wachezaji hawakuwa waangalifu katika dakika za mwanzo za mchezo huo na kuwafanya wenyeji watawale mchezo huo.


Kocha huyo wa zamani wa Mbeya City alisema kuwa kikosi hicho kilizinduka katika kipindi cha pili na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara lakini hayakuzaa matunda.

“Kipindi cha pili tuliamka lakini hatukufanikiwa kupata goli, kwa sababu mashambulizi yetu yalikuwa yanavurugwa na mwamuzi, kikubwa imepita na tunajipanga kuangalia mchezo unaofuata,” alisema Mwambusi.

Kikosi cha wawakilishi hao pekee wa Tanzania kwenye mashindano ya Yanga kiliondoka Algeria jana jioni na kurejea Uturuki kuendelea na mazoezi na kinatarajia kuwasili nchini Jumatatu.

0 comments:

Post a Comment