Saturday 18 June 2016

Mashabiki wa Croatioa waiweka timu yao kwenye mjadala mkubwa baada ya kirusha moto uwanjani.Fahamu zaidi hapa.

 Kocha wa Croatia Ante Cacic amewaita ‘magaidi wa michezo’ mashabiki waliorusha vipande vya moto uwanjani kwenye mchezo wao dhidi ya Jamhuri ya Czech.

Mchezo huo ambao umeisha kwa sare ya mabao 2-2, uliingia dosari mnamo dakika ya 86 wakati mashabiki wa Croatia waliporusha mafataki hayo kunako nyasi za dimba la Saint-Etienne.

Tayari Uefa wameshalitolea tamko na kusema kuwa watalifnyia uchunguzi suala hilo
“Hawa sio mashabiki halisi wa Croatia. Hawa watu ni hatari na mimi naweza kuwaita wahuni tu” Cacic amesema.

Croatia tayari wameshaadhibiwa na Uefa baada ya kundi kubwa la mashabiki wao kuleta vurugu katika mchezo wa ufunguzi wa kundi D dhidi ya Uturuki.

Kamati ya Maadili ya Uefa itakutana Jumamosi pale itakapokuwa tayari imepokea ripoti kamili juu ya vurugu hizo kutoka kwa kamishna wa mchezo na mwamuzi Clattenburg.

Cacic pia ana matumaini kwamba Chama Cha Soka nchini Croatia kitachukua hatua dhidi ya tukio hilo na kuongeza: “Asilimia 95 ya mashabiki wa Croatia wamepata aibu kubwa mbele ya mashabiki wa mataifa mengine.

“Hawa ni magaidi wa michezo. Pengine hili ni suala linalowahusu watu sita mpaka kumi. Natumaini kwamba watatambuliwa na kuchukuliwa hatua kali. Natumai Chama cha Soka cha Croatia wanafanya kila wawezalo kuhakikisha wanazuia hili.”

Wakati vurugu hizo zinatokea, Croatia walikuwa mbele kwa magoli 2-1, kabla ya Czech kusawazisha mnamo dakika ya 93 kufuatia mkwaju wa penati uliowekwa kimiani na Tomas Necid.

Wachezaji wa Croatia walionekana kuwashawishi mashabiki wao kuacha vurugu baada ya mchezo kusimama kwa dakika kadhaa na baadaye kuwatii na mchezo kuendelea.

“Tunapenda kuwaomba radhi Uefa, Jamhuri ya Czech na kila mmoja duniani kote ambaye ni mpenzi wa soka.” Amesema kiungo wa Croatia Ivan Rakitic.


0 comments:

Post a Comment