Tuesday 21 June 2016

Kocha wa zamani wa Azam FC kuifundisha Simba.Fahamu zaidi hapa.

ALIYEKUWA kocha mkuu wa timu ya Azam FC, Mcameroon Joseph Omog ameanza mazungumzo na uongozi wa klabu ya Simba kwa ajili ya kuja nchini kuifundisha timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

Simba imeanza mazungumzo na kocha huyo baada ya kocha chaguo la kwanza Sellas Tetteh, raia wa Ghana kuwapa masharti magumu, kabla ya kuzungumzia dau la mshahara analotaka kulipwa kila mwezi.

Mmoja wa viongozi wa juu wa Simba (jina tunalihifadhi) alisema kuwa klabu hiyo imechemsha kuendelea na mazungumzo na Tetteh kwa sababu alikuwa anauliza vitu ambavyo timu hiyo haina. Chanzo chetu kiliendelea kusema kuwa kutokana na mahitaji muhimu yaliyoulizwa na kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi) kukosekana, Simba iliamua kusitisha mazungumzo na mkongwe huyo.

“Huyo Mghana tumeamua kuachana naye, kuna vitu muhimu kupitia wakala wake tunaulizwa, hatuna, na yeye hawezi kufanya kazi kwenye mazingira ya kubabaisha, tumeona itakuwa ngumu kumpata kwa sababu hatuendani na hadhi yake, hatukufika kwenye suala malipo,” alisema kiongozi huyo. Aliongeza kuwa, suala la kocha msaidizi bado limewekwa kiporo mpaka kocha mkuu atakapopatikana.

“Kuhusiana na usajili, tumejipanga, tunafanya usajili kwa kushirikisha jopo na si mtu mmoja mmoja, wapo wachezaji na makocha wa zamani ambao wana mapenzi ya kweli na Simba,” kiongozi huyo alisema.

Wekundu hao wa Msimbazi pia walikuwa katika mazungumzo na Kalisto Pasua, lakini Mzimbabwe huyo ameikacha ofa ya Simba na kuendelea kuiongoza timu yake ya Taifa ambayo imefuzu kushiriki fainali za Kombe la Afrika mwakani. Simba ilimaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita nyumba na mabingwa Yanga na Azam.

0 comments:

Post a Comment