Wanasiasa
wakongwe nchini, Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar na Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika, kesho wanatarajia kuungana kwa mara ya
kwanza jukwaani tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Vigogo
hao wa vyama vya CUF (Maalim Seif) na Chadema (Lowassa) wataunguruma
katika viwanja vya Skuli ya Fuoni visiwani Zanzibar kumnadi mgombea
ubunge wa jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib
Ramadhani, katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januri 22 kuziba nafasi
ya aliyekua mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ally Tahir aliyefariki dunia
Novemba 11 mwaka jana.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu amesema kuwa chama chake kimemua
kuungana na CUF katika uchaguzi huo ili kuhakikisha mshirika wake huyo
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) anamshinda mgombea wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Aidha,
Mwalimu aliongeza kuwa baada ya Lowassa kushiriki uzinduzi wa kampeni
hizo kesho, viongozi wengine wa Chadema watafuata kwa kufanya mikutano
mbalimbali jimboni humo. Alisema kuwa baada ya Lowassa atafuata
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja Tundu Lissu kwa nyakati
tofauti, kisha wengine wataendelea hadi mwisho wa kampeni hizo.
Akizungumzia
uamuzi huo wa Chadema, Mkurugenzi wa Habari,Uenezi na Mawasiliano kwa
Umma, Salim Bimani alieleza kufurahishwa na uamuzi huo wa Chadema na
kueleza kuwa hatua ya Lowassa kuhudhuria uzinduzi huo itaongeza hamasa
kubwa kwa wapenzi wa chama hicho.
“Umenambia
hadi Lowassa atakuwepo? Ni furaha iliyoje, Wanzibari wana shauku
kumuona. Siku ya kampeni patakuwa hapatoshi Skuli ya Fuoni, hapa Simba
(Maalim Seif) kule Lowassa kipenzi kingine cha Wazanzibar,” Bimani
anakaririwa na Mwananchi.
Aliongeza
kuwa kama Lowassa atahudhuria mkutano huo atakuwa na mambo mawili
makubwa ya kufanya, la kwanza likiwa kuwashukuru Wazanzibar kwa kura
walizompa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Na la pili litakuwa
kumpigia kampeni mgombea wa CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani.
Lowassa
ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Maalim Seif ambaye ni
Katibu Mkuu wa CUF, wataingia katika jimbo hilo ikiwa ni siku chache
baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kufanya uzinduzi wa
kampeni hizo akiambatana na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho.
Hivyo,
kwa muktadha wa kisiasa, vigogo hao wa Ukawa wana kazi ya kusawazisha
matuta yaliyowekwa na timu ya chama tawala iliyoongozwa na Kinana.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment