Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Serikali
kupitia vyombo vyake vya Dola kutoa sababu za kufuta jalada la uchunguzi
wa Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa chama hicho, Ben Saanane ambaye
ametoweka tangu Novemba mwaka jana.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema jana
kwamba jeshi hilo linafanya kazi yake huku akihoji, “Chadema wamejuaje
kama hilo jalada la kesi ya Saanane limefutwa?
“Nenda kawaulize tena, wao wamejuaje, wakueleze vizuri hilo jalada limefutwa vipi na nani?”
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene
ilisema wanashangazwa na hatua iliyofikiwa na vyombo vya dola kufuta
jalada la uchunguzi wakati kada huyo bado hajapatikana mpaka sasa.
“Tunajua DCI (Robert) Boaz alisema hawako naye lakini tunashangazwa
na hatua yao ya kufuta jalada la uchunguzi mapema bila hatua nyingine,”
inasomeka taarifa hiyo.
Hivi karibuni, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja
wa Mataifa (UN) yenye makao yake makuu jijini Geneva, Uswisi, ilisema
iko tayari kutuma timu ya uchunguzi.
Chadema imerejea kauli yake ya kuitaka Serikali kutoa maelezo ya
wapi alipo Saanane iwe ndani au nje ya nchi kwani ndiyo yenye udhibiti
wa mipaka yote majini, nchi kavu na angani.
Makene alisema Serikali ina teknolojia ya mawasiliano ya kuweza
kujua na kupata mawasiliano ya mwisho ya mtu aliyewasiliana na kada
huyo, wakati gani na juu ya suala gani.
Makene alisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB),
imeshindwa kufanya kazi yake na kumaliza tofauti na sintofahamu
zinazoendelea.
Alisema ni aibu kwani taasisi za kimataifa zinaguswa na suala hilo huku vyombo vya usalama nchini vikikaa kimya.
Saanane, ambaye pia ni msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe, alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba 18 mwaka jana.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment