RAIS Abdi El-Fattah Al-Sisi wa Misri amesema nchi yake imejitoa kwa hali
na mali kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine za Afrika ili kujiletea
maendeleo ya kiuchumi kwa pamoja.
Alikuwa anazungumza na viongozi 37 wa vyombo vya habari kutoka nchi 27
za Afrika katika Ikulu ya mjini hapa, jana baada ya viongozi hao
kuhudhuria mafunzo ya wiki mbili juu ya Mwelekeo wa Vyombo vya Habari
Afrika kwa siku za usoni.
“Misri sasa inarudi tena barani Afrika na sera ya ushirikiano wa
kuimarisha uchumi na ndugu zake wa nchi za Afrika ili kujiletea
maendeleo,” alisisitiza.
Alisema Misri tayari inashirikiana na nchi mbalimbali barani katika
nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na za kilimo, elimu na afya na kwamba
sasa ipo haja ya kupanua zaidi kuimarisha ushirikiano huo katika
miradi, uwekezaji na ujenzi wa miundombinu.
“Miradi ya kuunganisha barabara, ujenzi wa reli na usafiri wa majini ni
muhimu katika kuimarisha usafirishaji wa bidhaa na mawasiliano na hivyo
kukuza uchumi baina ya nchi,” alieleza.
Alikumbusha kuwa, kipindi cha kupigania uhuru kilishapita na kwamba sasa
Afrika iko katika kipindi kingine cha kuimarisha uchumi wake na moja ya
njia ya uhakika katika kutekeleza hilo ni kuboresha ushirikiano.
Alifafanua kwamba katika sera ya nchi yake ya kurejea Afrika, nchi yake
haitafuti uongozi, bali ushirikiano wa kweli utakaoziongoza nchi za
Afrika kuwa na lugha moja ya kushirikiana kwa kujiletea maendeleo.
“Tumerudi kwa ndugu zetu Afrika ili tushirikiane katika kujenga mataifa yetu kiuchumi,’’ alisisitiza Rais Al-Sisi.
Sera ya mambo ya nje ya Misri kwa muda mrefu imekuwa ikijielekeza kwa
nchi za Mashariki ya mbali kutokana na ukaribu wa kijiografia na
kiutamaduni, lakini sasa inajitahidi kurejea barani kwake Afrika
kuimarisha ushirikiano.
Katika suala la vita dhidi ya ugaidi, Rais huyo alisema nchi yake kama
ilivyo kwa mataifa mengine inapigana dhidi ya ugaidi na kwamba inatoa
mafunzo kwa ajili ya watu wake pamoja na nchi nyingine barani Afrika ili
kukabiliana na hali hiyo ya tishio la kiusalama.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza HapaFollow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment