Askofu
Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, amezindua
operesheni mpya aliyoipa jina la ‘Operesheni 81Mzizima’ huku akimtaka
mtu anayeitwa Daud Bashite ajitokeze hadharani kuthibitisha uhalali wa
vyeti vyake.
Hivi
karibuni, Askofu Gwajima alihubiri kanisani kwake na kusema Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, anatumia vyeti vya mtu anayeitwa
Paul Christian, wakati jina lake halisi ni Daud Albert Bashite.
Akizungumza
wakati wa ibada kanisani hapo, Ubungo jijini Dar es Salaam jana,
Askofu Gwajima alisema operesheni hiyo mpya ni vita ya mwisho ya
kumshikisha mtu adabu.
Alisema,
tangu aanzishe hoja hiyo, hadi sasa wahusika hawajajitokeza hadharani
kujibu tuhuma hizo, jambo ambalo alisema linaonyesha alichokisema ni
kweli.
“Tangu niibue hoja ya Makonda anatumia vyeti vya Daud Albert Bashite, hakuna aliyejitokeza hadharani kukanusha madai yangu.
“Mimi
naamini nilisema ukweli kwani kitendo cha kukaa kimya kinaonyesha wazi
kuwa ni kweli ninachokisema na kama anabisha, aje hadharani kukanusha
akiwa na vyeti vyake na mimi nitakuja na vyangu…
“Kuna baadhi ya watu wananisihi sana niache kumchambua eti wanasema, Gwajima acha, hiyo inatosha.
“Mbona wakati Makonda aliponihusisha na dawa za kulevya hakuna aliyejitokeza kumwambia aache?
“Hii ni vita ya mzizima ya kushikisha adabu iitwayo hold the final battle of good manners,”alisema Askofu Gwajima.
“Hizi
ni salamu tu ili ajue kuwa ukimshambulia baba wa imani, hauwezi kubaki
salama kwa sababu viongozi wa dini wanapigana vita mbalimbali ikiwamo
majini na mashetani, lakini wanashinda kwa jina la Yesu.
“Nina uhakika na nina ushahidi usio na shaka kuhusiana na suala hilo, labda ajitokeze na kuniomba msamaha.
“Nina material na mazagazaga kibao kuhusu Daud Bashite, niseme,” alihoji Gwajima huku waumini wake wakiitikia semaaa.
“Lakini,
kwa leo sitaki nimwongelea sana, kwa sababu namwonea huruma, ila
ninachotaka kumwambia ni kwamba, usiweke miguu yako kwenye mashine ya
kusaga na kukoboa, utageuka sembe.
“Akumbuke
kuwa, baba wa familia akiguswa, hata watoto wanaamka, ndicho
kilichojitokeza katika maisha yangu kwani baada ya kushambuliwa sana,
waumini wameongezeka tofauti na awali.
“Hata wale waliokuwa hawaji kanisani, hivi sasa wanakuja,”alisema.
Katika
mahubiri hayo, Askofu Gwajima alisema kuna wakati Mungu huwainua watu
wake kwa makusudi maalumu ili kutimiza kusudio lake.
“Sasa nataka kumwambia kuwa, hizi ni salamu tu, nimerusha ka kipande tu… kuhusu Bashite, lakini kelele kibao.
“Hapa
sitaki maigizo wala ngonjera, ninachotaka ni samahani tu, lakini
anapaswa kujua kuwa, ukimshambulia baba wa imani, awe askofu, mchungaji,
padri au wa dini yoyote, hauwezi kubaki salama, lazima na wewe
utashambuliwa tu,”alisema.
Pamoja
na hayo, alisema kama ataamua kukaa kimya kama anavyoombwa na baadhi ya
watu, akikaa kimya Mungu atawainua watu wengine ili waweze kuzungumza
kwa niaba yake.
Kwa
mujibu wa Gwajima, hana nia ya kumchafua mtu kwenye suala hilo wala
hana mgogoro na hana tatizo, ila aliamua kusema alichokisema kwa sababu
alichokozwa.
“Nilichokozwa na siwezi kunyamaza kwa sababu ninachokisema ni kweli na wala hakiwezi kubadilika leo, kesho wala keshokutwa.
“Sijawahi kumpiga mtu bila kunichokoza na wala sijawahi kumchokoza muumini wangu kanisani, awe muislamu au mtu mwingine.
“Sisi
ni wakristo, lakini waislamu ni ndugu na marafiki zetu. Hivyo, basi
hakuna mshale utakaoweza kunipiga mimi na vita kwangu haijaanza leo wala
jana,”alisema.
Pia,
Askofu Gwajima alisema ana historia ndefu inayoanzia Oktoba 21, mwaka
1996 wakati alipoanzisha kanisa lake na kupitia changamoto mbalimbali
ambazo alizishinda kwa nguvu za Mungu.
Alisema
kwamba, hadi sasa ana makanisa 400 yaliyopo maeneo mbalimbali ndhini na
mengine 300 yaliyopo katika nchi mbalimbali duniani.
Katika
mabuhiri hayo, Askofu Gwajima alimtolea mfano Erick Shigongo kwa kile
alichosema kuwa ni miongoni mwa watu wa kuigwa kwani wanatafuta
mafanikio kadri wawezavyo.
“Mtu
ukipata mafanikio kunakuwa na chuki kibao zinazotolewa ili wakuvunje
moyo badala ya kukaa na kuanza kutafakari ili kuona umewezaje ili
wakuige.
“Mwisho
naamini utafiti unapingwa kwa utafiti, hivyo basi kauli yangu kwa Daudi
itapingwa kwa vielelezo ili na mimi niweze kutoa vielelezo vyangu,” alisema Askofu Gwajima.
Wiki
iliyopita Jeshi la Polisi kwa mara nyingine lilizingira nyumba ya
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kwa kile
lilichodai kuwa lilifika kufanya uangalizi.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment