Mahakama Kuu Kanda ya Arusha leo inatarajiwa kusikiliza maombi ya
dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambaye
amekuwa akiisaka kwa miezi minne sasa.
Mbunge huyo ambaye
amekamatwa tangu Novemba 2 mwaka jana akiwa bungeni Dodoma, amewekwa
mahabusu katika Gereza la Kisongo, Arusha.
Jaji Salma Magimbi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ndiye atakayesikiliza rufaa hiyo namba 126
ya mwaka jana ambayo iliwasilishwa na mawakili wanaomtetea, Kibatala,
John Mallya na Sheck Mfinanga.
Maombi hayo yanatokana na
mapingamizi ya kisheria yaliyowekwa na Serikali mara baada ya uamuzi
uliotolewa Novemba 11 mwaka jana na Hakimu Mkazi Arusha, Desderi
Kamugisha kumpa dhamana katika kesi inayomkabili ya kutoa kauli za
uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
Hata hivyo, Lema alikwama
baada ya mawakili wa Serikali kuwasilisha kusudio la kukata rufaa.
Mawakili wa Lema waliwasilisha Mahakama Kuu, maombi ya kutaka mapitio ya
kesi hiyo, lakini yalitupwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Sekela Moshi
kutokana na upungufu na kutakiwa kukata rufaa.
Walifanya hivyo Desemba 2 mwaka jana lakini maombi yao yalitupwa kutokana na mapingamizi ya mawakili wa Serikali.
Waliomba
kuongezewa muda wa kukata rufaa na Desemba 20 mwaka jana na Jaji
Modesta Opiyo alikubali maombi hayo na kutupa mapingamizi ya Serikali.
Hata
hivyo, siku ambayo ilipangwa Jaji Maghimbi kutoa uamuzi juu ya rufaa
hiyo Jamhuri iliwasilisha notisi ya kupinga kusikilizwa.
Jaji Magimbi alisema kutokana na hilo, rufaa nyingine zitasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.
Februari
27, mapingamizi yote ya Jamhuri yalitupwa na Mahakama ya Rufaa, baada
ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuondoa mapingamizi hayo.
Majaji
waliotupa mapingamizi hayo ni Bernard Luanda, Kipenka Mussa na Stela
Mugasha ambao walieleza kusikitishwa na mwenendo wa kesi hiyo.
Katika
kesi ya msingi, Lema anatuhumiwa kuwa kati ya Oktoba 23 hadi 26 mwaka
jana alitoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais Magufuli katika maeneo
tofauti katika mikutano yake ya hadhara.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment