Hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutoa siku 14 kwa
Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) na taasisi za Serikali kuhakikisha
wanalipa madeni yao ya umeme la sivyo watakatiwa umeme, vitaipa wakati
mgumu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka aliwaambia
waandishi wa habari kwamba shirika lake linadai wateja hao jumla ya
Sh275 bilioni.
“Tunadai kiasi kikubwa sana cha fedha kutoka kwa wateja wakubwa na
wadogowadogo, mpaka Zeco, hivyo tunatoa notisi ya siku 14 kuanzia leo
(jana) walipe deni lao kwani baada ya hapo tutasitisha huduma pamoja na
kuchukua hatua nyingine za kisheria,” alisema Dk Mwinuka.
Katika kiasi hicho, Zeco inadaiwa Sh127 bilioni ambacho ni sawa na
asilimia 15 ya Bajeti ya Serikali ya Zanzibar kwa mwaka 2016/17 ambayo
ni Sh841.5 bilioni.
Pia kiasi hicho ni kikubwa karibu mara nne ya kile kilichotengwa
katika bajeti hiyo kwa ajili ya mikopo ya ndani ambacho ni Sh33.0
bilioni hali inayoonyesha kwamba Zeco na SMZ watalazimika kuandaa mpango
mkakati wa kulipa deni hilo ambao utamaanisha kujifunga mkanda ili
kulimaliza.
Alipoulizwa kuhusu notisi hiyo ya kulipa deni, Waziri wa Ardhi,
Maji, Nishati na Mazingira wa Zanzibar, Salama Aboud Talib ambaye
alikuwa ziarani Pemba alisema hadi jana hakuwa amepokea barua kutoka
Tanesco hivyo asingeweza kuzungumza chochote.
Wiki iliyopita, akiweka jiwe la msingi katika kituo cha kupoza
umeme cha njia ya Kv 132 mkoani Mtwara, Rais John Magufuli aliiagiza
Tanesco kuwakatia umeme wadaiwa wote sugu ikiwamo Zanzibar. Alisema
shirikia hilo halipo kisiasa, hivyo wadaiwa wote wakatiwe umeme.
Sambamba na hayo, alilitaka shirika hilo kutoingia mikataba na
kampuni zinazoweza kusababisha au kuongeza madeni, badala yake mwekezaji
yeyote akitaka kuwekeza azalishe umeme wake na kuuza mwenyewe.
Wadaiwa wengine
Kuhusu wadaiwa wengine, Dk Mwinuka alisema hadi kufikia Januari,
shirika hilo lilikuwa linazidai wizara na taasisi za Serikali kiasi cha
Sh52 bilioni huku kampuni binafsi na wateja wadogo wakidaiwa jumla ya
Sh94 bilioni.
Alisema malimbikizo hayo ya madeni yamekuwa yakikwamisha jitihada
za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya msingi ndani ya shirika kwa
wakati ikiwamo uendeshaji, matengenezo ya miundombinu pamoja na miradi
mbalimbali.
Alisema kulipwa kwa malimbikizo hayo ya madeni kutaisaidia Tanesco
kujiendesha kiushindani na kwa ufanisi zaidi, hivyo kuendelea kuchochea
kasi ya ukuaji sekta mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme nchini.
Alipoulizwa kuhusu mashirika na taasisi za umma zinazodaiwa
malimbikizo hayo ambayo Tanesco haikuyataja, Msemaji wa Serikali, Dk
Hassan Abbas alisema mashirika hayo yanatakiwa kuanza kutekeleza agizo
hilo kwa kulipa deni kama wanavyodaiwa.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment