Wednesday 16 March 2016

#YALIYOJIRI>>>Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), David Mattaka Ashitakiwa Tena Kwa Uhujumu Uchumi.Fahamu zaidi hapa.

Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka na wenzake wawili wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kuisababishia hasara Serikali kupitia ukodishaji wa ndege.

Wakili Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis akishirikiana na mawakili wa Takukuru, Joseph Kiula na Stanley Luoga waliwataja washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage kuwa ni Ofisa Mtendaji Mkuu Mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Ramadhan Mlinga na Mwanasheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka.

Wakili Vitalis alidai kuwa Oktoba 9, 2007 katika ofisi za ATCL zilizopo wilayani Ilala, Mattaka alitumia vibaya madaraka kwa kutia saini mkataba wa ukodishaji wa ndege A320-214 iliyotengenezwa kwa namba 630 baina ya Wallis Trading Inc na ATCL.

Alidai alifanya hivyo bila ya kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma na taratibu za zabuni kwenye mchakato huo.

Pia, alidai Oktoba 27, 2007 alitumia vibaya madaraka yake kwa kutia saini cheti cha kuruhusu mchakato wa ukodishaji wa ndege hiyo bila ya kufuata ushauri wa kiufundi aliopewa na kuisababishia Serikali hasara ya dola 772,402.08 za Marekani zilizolipwa kwa kampuni ya Aeromantenimiento,S. A kama gharama za huduma ya matengenezo.

Kuhusu Mattaka, wakili huyo alidai Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kumpa dhamana na kwamba, anaweza kuomba kudhaminiwa kupitia Mahakama Kuu.

Washtakiwa Mlinga na Bertha wanadaiwa kuwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA walighushi muhtasari wa kikao cha siku ukionyesha mamlaka hiyo ilijadili maombi ya ATCL juu ya kuidhinishwa kwa mkataba huo.

Washtakiwa hao walikubaliwa dhamana kwa kuwa shtaka linalowakabili linadhaminika.  Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 29.

0 comments:

Post a Comment