Wednesday 16 March 2016

DNA YA MKEMIA MKUU NA BAO LA KELVIN YONDANI.FAHAMU ZAIDI HAPA.

Na Zaka Zakazi
Disemba 21 mwaka jana, mkemia mkuu waserikali, Profesa Samwel Manyele, aliistua nchi pale alipotoa ripoti ya matokeo ya uchunguzi wa makosa ya vinasaba (DNA) yaliyowasilishwa katika ofisi ya wakala wa maabara yake kwa mwaka huo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto 49 kati ya100, hawakuwa watoto halali wa baba anayedhaniwa kuwa ni baba mzazi!

Endapo uchunguzi kama huu ungefanyika kwenye magoli yanayofungwa kwenye mpira wetu hapa nchini hasa ligikuu ya Vodacom, ingebainika kwamba baadhi yake siyo halali kwa wafungaji waliotajwa. Mfano rahisi ni goli la kwanza la Yanga dhidi ya African Sports, March 8 mwaka huu, uwanja wa taifa jijini Dar Es Salaam.

Dakika ya 33 ya mchezo, Kelvin Yondani akiwa nje ya eneo la hatari la Africans Sports, alipokea pasi kutoka kwa Deus Kaseke na kuachia shuti lililombabatiza Thaban Kamusoko na kutinga wavuni.

Kiutaratibu, bao hili lilipaswa kuhesabiwa la Thaban Kamusoko huku Kelvin Yondani akihesabiwa kama mtoa pasi ya mwisho kwasababu Kamusoko ndiye mchezaji wa mwisho wa Yanga kuugusa mpira kabla haujatinga wavuni.

Lakini mwamuzi wa akiba, Frank Komba kutoka Dar Es Salaam, ambaye kimsingi ndiye mwenye mamlaka ya kutoa ripoti ya mchezo yakiwemo mabao, alilihesabia bao hilo kwamba limefungwa na Kelvin Yondani.

Hoja ya mwamuzi huyu mwenye beji ya FIFA ilikuwa kwamba, hata bila kumgonga Kamusoko, ulempira ungeenda golini kwahiyo Kamusoko hawezi kuhesabika kama mfungaji, hapa kaka Komba, aliteleza!
Nasema aliteleza kwasababu alitumia tafsiri ya bao la kujifunga kuamua mfungaji wa bao hili.

Tafsiri ya bao la kujifunga ni kwamba, endapo mchezaji watimu A amepiga mpira kuelekea lango la timu B, ule mpira ukambabatiza mchezaji wa timu B na kutinga wavuni kinachoangaliwa ni ‘Je, bila kumbabatiza mchezaji wa timu B mpira ungelenga lango au ungetoka nje?.’  Kama ungetoka nje basi hilo ni bao la kujifunga, kama ungelenga lango basi mpigaji wa shuti la awali huhesabiwa ndiyo mfungaji.

Bahati mbaya kwa kaka Komba na wadau wengine wanao husika na soka wakiwemo waandishi wa habari ni kwamba, matukio kama haya hutokea marachache sana kiasi kwamba yanapotokea huwakuta wakiwa hawajajiandaa.

Kwamfano, kulipata bao kama la Yondani na Kamusoko inabidi urudi nyuma mpaka Mei 23, 2007 kwenye fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya kati ya AC Milan na Liverpool. Mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Andrea Pirlo, ulimgonga Philipo Inzaghi na kutinga wavuni, bao likahesabiwa la Inzaghi na Pirlo akahesabiwa ametoa pasi ya mwisho.

Hivi karibuni, Lionel Messi na Luis Suarez wa Barcelona walipiga penati ambayo iliwachanganya watu wengi wakiwemo waamuzi wakubwa. Kuna mwamuzi mmoja wa FIFA hapa nchini (jina nalihifadhi) alisema inabidi akazipitie sheria upya ili ajiridhishe.

Sasa mwamuzi huyu angetokewa na tukio kama lile wakati akiwa uwanjani angefanya nini? (nikawaza kimyakimya).
Nilichojifunza ni kwamba, tatizo hili halipo kwa waamuzi tu bali hata waandishi (siyo wote lakini).

Kwamfano, kwenye mchezo wa sare ya 2-2 kati ya Azam FC na Yanga March 5 mwaka huu, mwamuzi msaidizi namba moja, Sudi Lila, alilikataa bao la Azam.

Sitaki kujikita kujadili utata wa bao hilo bali nataka kuangalia namna lilivyonisaidia kubaini tatizo la asilimia 49 ya DNA za magoli kwa waandishi na wachambuzi wetu.

Vyombo vingi vya habari vililiripoti kwamba bao lile lilifungwa na Shomari Kapombe na kuna gazeti lilimnukuu Kapombe mwenyewe akilalamika kwamba anavunjwa nguvu katika kuwa nia kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora.

Makala nyingi za wachambuzi ambao wengi wao ni waamuzi wastaafu, waandishi au wachezaji wa zamani na makocha, zililielezea bao lile kwamba lilifungwa na Shomari Kapombe.
Lakini kwa hali halisi, bao lile halikufungwa na Shomari Kapombe bali lilikuwa bao la kujifunga la kipa wa Yanga, Ally Mustapha “Barthez”.

Kichwa cha Shomari Kapombe kiligonga nguzo na kurudi ndani, Barthez akakutana na mpira uliokuwa ukirudi, ukamgonga na kuingia wavuni…hayo ndiyo mabao ya kujifunga na hapa ndipo ile tafsiri aliyoitumia kaka Lila kwenye bao la Kamusoko, ilipokuwa ikihitajika zaidi.

Ili kuweza kukabiliana na matukio kama haya ambayo hutokea kwa nadra, waamuzi wetu wanatakiwa wawewanasoma ‘sana’ sheria mara kwa mara. Sisemi kwamba kwasasa hawasomi..hapana. Najua wanasoma, lakini siyo‘sana’…wao wanachokifanya ‘sana’ ni kujenga na kuimarisha utimamu wao wa mwili.

Kwenye nchi za wenzetu, huwa kunakuwa na kamati maalumu ambazo hupitia matukio mbalimbali na kuyafanyia maamuzi, likiwemo tukio kama hili.

Kwa mfano, kwenye kombe la dunia la 2002, mchezo wa mwisho wa makundi kundi C kati ya Brazil na Costa Rica, Ronaldo De Lima alifunga bao la kwanza ambalo “Frank Komba wa siku hiyo” alilihesabia kama bao la kujifunga la mlinziwa Costa Rica, Luis Marin
Ronaldo aliuwahi mpira wa krosi ya chinichini kutoka wingi ya kushoto na kuupiga mpira ambao beki (Marin) aliingiza mguu kuzuia lakini ukamgonga na kutinga kimiani.

Alipogundua bao hilo lilihesabiwa la kujifunga, Ronaldo alikasirika na kumfuata mwamuzi wa akiba (Frank Komba wa siku hiyo) na kumlalamikia.

Baadaye  FIFA walikaa na kuliangalia upya goli lile na kuamua kwamba lilikuwa bao hahali la Ronaldo kwasababu shuti lake lililenga lango hata kama beki yule asingeugonga mpira ule.

Ronaldo alikuwa akifukuzana na Miroslav Klose wa Ujerumani kuwania kiatu cha ufungaji bora na mpaka wakati huo, Ronaldo alikuwa na mabao matatu huku Klose akiwa na manne.

Bao hilo likamfanya Ronaldo alingane na Klose na mwisho wa mashindano akawa mfungaji bora akiwa na mabao manane.

0 comments:

Post a Comment