Thursday 27 July 2017

WAZIRI Mkuu Avishukia Vyuo Vinavyolalamika Kwa Kufungiwa na TCU.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha kwamba programu zote zinazotolewa na taasisi za elimu ya juu zinawawezesha wahitimu kujiajiri na kuwa na sifa za ushindani katika soko la ajira kimataifa.

Amesema wakati umefika sasa kwa wasomi katika vyuo vyetu vikuu tujiridhisha kuwa mitaala inayotolewa kama inawaandaa wahitimu kupata taaluma na stadi za kuweza kujiajiri na kupambana na changamoto za kimaisha.

Amesema taasisi za elimu ya juu nchini ziangalie mitaala yake na kuimarisha mfumo wa ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ili kwenda sambamba na dunia ya kazi inayoendana na agenda ya maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Julai 26, 2017) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 12 ya Elimu ya Juu, jijini Dar es Salaam ambapo amevutaka vyuo hivyo badala ya kuendelea kulumbana kwenye makongamano na vyombo vya habari, vifanye maboresho yanayotakiwa ili viweze kuendelea na ufundishaji. Aidha amesema kuwa, lengo la serikali ni kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na kwamba maboresho yanayotakiwa kufanyika yanawezekana.

Waziri Mkuu amesema maonesho hayo ni jukwaa la kipekee ambalo litaibua mjadala sahihi kuhusu uhalali wa kozi zinazotolewa na vyuo husika vya elimu ya juu. “Hivyo mnayo nafasi ya kuonesha kwa vitendo uwezo wenu katika utafiti, ubunifu na matumizi ya sayansi na teknolojia zinazotumika katika maendeleo ya viwanda.”

Amesema ni vema mfumo wa ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ukaimarishwa ili kuhakikisha asilimia 60 ya wanafunzi wanahitimu shahada kwenye sekta ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi.

Amesema taasisi za elimu ya juu ziweke mikakati ya kuinua na kuboresha taaluma wanayoitoa ili ilete tija kwa maendeleo ya Taifa na Dunia. Pia kuanzisha program za mafunzo zenye kukidhi mahitaji na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuzingatia mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amezitaka taasisi hizo kuendelea kuimarisha mfumo wa udahili na kujipanga kutumia fursa za elimu na mafunzo ndani na nje ya nchi kwa makundi yote ya jamii kwa usawa katika ngazi zote hususan ufundi, hisabati, sayansi na teknolojia.

Pia Waziri Mkuu amesema ni wakati muafaka kwa taasisi za elimu ya juu nchini kuandaa mikakati ya kuongeza udahili kwa kuzingatia mahitaji ya rasilimali watu na ujuzi unaohitajika katika sketa zinazokua haraka mfano mafuta, gesi na madini.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, JULAI 26, 2017

Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment