Wednesday 14 February 2018

Serikali Yataja Maeneo Yanayotumika Kupitisha Dawa za Kulevya.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imebaini maeneo ya bahari kuu, bandari, vituo vya mabasi na viwanja vya ndege ndio yanatumika zaidi kupitisha dawa za kulevya.

Amesema wafanyabiashara, wasambazaji na watumiaji wa dawa hizo wameendelea kukamatwa lengo likiwa ni kuhakikisha biashara hiyo inamalizika nchini.

Taarifa iliyotolewa leo Februari 13, 2018 na ofisi ya Waziri Mkuu imesema kuwa kiongozi huyo ametoa kauli hiyo wakati akikabidhi gari kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Amesema mbali na kukamata meli, pia Serikali imewakamata wasambazaji pamoja na kundi kubwa la wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hiyo sambamba na watumiaji.

Waziri Mkuu amesema lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na kizazi chenye uwezo wa kuzalisha mali.

Amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya, ambapo hivi karibuni imekamata meli nyingi, moja ikiwa inatokea pwani ya Msumbiji na ilikamatiwa maeneo ya Mtwara ikiwa na dawa nyingi za kulevya.

“Ni wakati wa Serikali kuendelea kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na leo hii tunawakabidhi gari hili jipya kabisa ili iweze kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo,” amesema

Pia, amewataka Watanzania waachane na biashara ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kazi ya kusambaza, kuzalisha na kutumia na watakaokamatwa wakijihusisha nazo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Amesema kwa sasa Serikali inajenga maabara ambayo itatumiwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa dawa wanazozikamata.

Ameongeza kuwa wananchi wanatakiwa kushirikiana na Serikali katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa mara wanapowabaini wafanyabiashara, watumiaji na wasambazaji wa dawa hizo.

Pia wahakikishe wanawalinda vijana ili wasijihusishe na dawa za kulevya.

Kwa upande wake, Sianga ameishukuru Serikali kwa kuipatia mamlaka hiyo gari ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi waachane na biashara hiyo huku akiwasihi kupambana kuhakikisha dawa za kulevya haziingii nchini.

Amesema mbali na kudhibiti biashara hiyo, pia wanatoa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya vikiwemo vitendo viovu vinavyofanywa na watumiaji ili wachukie na waache kutumia dawa hizo. 

Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment