Wednesday 28 February 2018

CCM na Polisi Wapangua Tuhuma za Freeman Mbowe.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameibua tuhuma mpya dhidi ya baadhi ya idara za Serikali ikiwamo polisi akidai kuna mkakati wa kuwafungulia kesi ya uhaini, mauaji na ugaidi viongozi wa chama chake.

Pia, ameinyooshea kidole CCM akidai kwamba inatafuta umaarufu kwa nguvu kwa kununua madiwani.

Hata hivyo, polisi na CCM wamekana tuhuma hizo na kumtaka Mbowe aache siasa za malumbano.

Mbowe alitoa kauli hiyo jana katika mkutano na waandishi wa habari, muda mfupi kabla ya kuwaongoza viongozi wa chama hicho kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kuhojiwa kwa madai ya kufanya maandamano kinyume cha sheria na kuachiwa kwa dhamana.

Wakati Mbowe akieleza hayo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema tuhuma dhidi ya polisi si za kweli na ndio maana viongozi hao walifika kituoni hapo kwa ajili ya kuhojiwa.

“Tutaendelea kuwahoji hawa viongozi kwa kufanya maandamano bila ya kuwa na kibali jambo ambalo ni kosa,” alisema Mambosasa.

Mbali ya Mambosasa, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole pia alimjibu akisema, “Mbowe na viongozi wenzake wa upinzani wafanye siasa safi na watoe uongozi bora. Waache siasa za matukio na uchochezi kwa sababu hazibadilishi maisha ya watu. CCM tumeamua, hasa Awamu ya Tano kushughulika na shida za watu na kuwaletea maendeleo.”

Alichokisema Mbowe

Mbowe alidai kwamba mkakati wa kuwafungulia kesi hizo unatokana na matukio mbalimbali yaliyotokea ya mauaji na utekaji huku akidai vyombo vya dola vinashindwa kutimiza wajibu wake hivyo kujenga chuki miongoni mwa jamii.

Alisema kuna matukio yaliyojitokeza katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni uliofanyika Februari 17 yalisababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini (22) na wanachama watano wa Chadema kupigwa risasi za moto.

Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi Februari 16 akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni wakati polisi wakiwazuia wafuasi na viongozi wa Chadema waliokuwa wakiambatana kwenda ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa Kinondoni kushinikiza kupewa viapo vya mawakala wao.

Siku nne baadaye, Mambosasa aliwataka viongozi saba wa Chadema kufika polisi kwa mahojiano.

Mbowe alisema, “Wanatafuta namna ya kutubambika kesi za kigaidi, mauaji au za kihaini... ni mkakati wa kweli na tunamweleza Rais, hatutarudi nyuma katika kutetea demokrasia ya kweli. Mpaka sasa wanachama wetu watano kati yao wawili ni wanawake waliopigwa risasi za moto hawataki kuwapatia dhamana, wanajua wakitoka wataongea yaliyowasibu ndio maana hawataki kuwaachia wala kuwapeleka mahakamani.”

Mbowe aliendelea kutuhumu, “Risasi hizo zilielekezwa kwetu, sitaki kusema mimi ila hii si Tanzania tunayoitambua... Tumeanza kuzoea kuuana, kuumizana na wanasababisha machafuko na haya ni maonevu na haya mambo hayakuwapo zamani, tujiulize kwa nini yanatokea sasa?

“Hizi chaguzi zitaendelea kuzaa majeraha na maumivu kwani wanaosababisha wanalindwa na viongozi wa juu. Haiwezekani mawakala wetu hadi siku ya mwisho walikuwa hawajapata hati ili waibe kura na ndicho walichokifanya.”

Kuhusu madai ya kuwapo kwa mkakati wa kuifuta Chadema, Mbowe alisema unaweza kufanikiwa lakini athari zake zitakuwa ni kubwa kwa Taifa, “Wataiua Chadema lakini si mioyo ya watu, utaiua CUF na vyama vingine si hisia za watu na unapoziua taasisi kama hizi zinazowasemea watu wanatengeneza magenge huko na wataunda vikundi vya kigaidi ambavyo ni hatari zaidi.

“Chama hiki si cha kigaidi ni chama cha mikusanyiko ya watu wengi na CCM kama wanataka kurudisha imani kwa wananchi wasifanye hivyo kwa kununua madiwani, wafanye mambo yanayoeleweka na watakubalika.”

Alikuwa akizungumzia barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliyoiandikia Chadema akitaka ijieleze kutokana na madai ya uvunjifu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na ile ya maadili kwa kufanya maandamano Februari 16.

Barua hiyo ya Februari 21, iliyokuwa ikitakiwa kujibiwa kabla ya Februari 25, Jaji Mutungi katika sehemu ya barua hiyo alisema licha ya tuhuma hizo kuwa zinafanyiwa kazi na taasisi zingine za Serikali, hata ofisi yake kwa namna moja au nyingine anaweza kulishughulikia.

“Hivyo, kwa barua hii, nakitaka chama chenu kuwasilisha maelezo ya kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria, kwa kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, kwa kuchochea wananchi kuandamana bila kufuata utaratibu wa sheria na kufanya vurugu,” ilieleza sehemu ya barua hiyo ambayo tayari Chadema ilishasema kuwa imeijibu.

Hukumu ya Sugu

Mbowe alizungumzia hukumu ya mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga iliyotolewa juzi ya kuhukumiwa miezi mitano jela akidai ni mkakati ovu uliopagwa.

“Tunaheshimu sana Mahakama na Mahakama inapaswa kuheshimiwa lakini mawakili mmojammoja wanapofanya makosa wanaichafua Mahakama. Jaji Mkuu (Profesa Ibrahim Juma) alisema wanasiasa tusiingilie Mahakama, hatutaisema vibaya au kuihukumu hapana, tunawahukumu watendaji wa mahakama,” alisema Mbowe.

“Hukumu hii tuliijua siku nne kabla na mtakumbuka hakimu (Michael Mteite) tulimkataa toka mwanzo na sisi kama Chadema hatutaki kusema hatuna imani na Mahakama, lakini Jaji Mkuu kama alivyosema tusiingilie Mahakama na Jaji Mkuu anapaswa kujua hili na kama anataka kuanza, basi aanze na kesi hii ya Mbeya.”

Mbowe alisema amekuwa akiombwa na wanachama na wananchi kutoa kauli ya kulipiza kisasi kwa yanayowakuta lakini alisisitiza kwamba hatafanya hivyo akisema kutofautiana kiitikadi si kigezo cha kusababisha uvunjifu wa amani.

“Tupambane na watawala waovu na si wananchi kwa wananchi na wanaostahili kulaumiwa ni Serikali. Wanachama wa Chadema waendelee kuwa makini, tuchukue kila tahadhari kwani vyombo vinavyopaswa kutupa ulinzi havifanyi hivyo,” alisema Mbowe.

Majibu ya Mambosasa

Hata hivyo, Kamanda Mambosasa alisema tuhuma za Chadema dhidi ya jeshi hilo hazina mashiko huku akisisitiza kuwa polisi wanafanya kazi yao kwa weledi na ndiyo maana viongozi hao walikuwa wakihojiwa kituoni hapo.

“Muwaulize hao Chadema kwa nini tuhuma wazielekeze jeshi la polisi? Wao wenyewe wanajua ndiyo maana leo (jana) hii tunaendelea kuwahoji kwa kufanya maandamano bila ya kuwa na kibali jambo ambalo ni kosa,” alisema Mambosasa.

Polepole amjibu Mbowe

Polepole alipotafutwa kutoa maoni yake juu ya kauli hizo za Mbowe alisema, “Hatuna muda wa kulumbana siasa za madaraka. Mbowe asitafute mchawi nje ya chama chake na yeye mwenyewe. Anayetuharibia wigo wa demokrasia sasa hivi ni mtu ambaye anazungumza masuala ya kuhamasisha na kuleta taharuki. Anazungumzia kubeba majeneza ya Watanzania, mbona hajazungumza kubeba majeneza ya watoto wake. Mbona hasemi watoto wake wako wapi? Anapiga mawe polisi na kuandamanisha watu lakini watoto wake wako salama.”

Alisema siasa za namna hiyo hazileti maendeleo katika Taifa na kwamba CCM sasa inafuatilia kazi ambayo iliwaahidi Watanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Polepole pia alizungumzia madai ya Mbowe kuhusu hukumu ya Sugu na kusema, “Mtu kigeugeu ni mbaya sana. Mahakama ikiamua yeye mbunge wake halali, mahakama nzuri. Mahakama ikimhukumu mbunge wake Sugu na wengine wanaotoa lugha ya uchochezi na uongo na wanashindwa kuthibitisha, mahakama mbaya. Huo si ustaarabu wa uongozi ni ukigeugeu wa kisiasa.”

Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment