Saturday 28 January 2017

Mume na mmiliki wa Famasi Watiwa mbaroni Kwa Kusababisha Kifo cha mjamzito.Fahamu zaidi hapa.

Watu  wawili, akiwemo mmiliki wa duka la dawa muhimu za binadamu katika kijiji cha Itagata wilayani Manyoni, wanashikiliwa na Polisi mkoani Singida kwa tuhuma za uzembe wa kusababisha kifo cha mjamzito, Heleni Maduhu (29).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni mume wa marehemu, Bahame Kamuda (32) na Joseph Hengwe (50) ambaye ni mmliki wa duka la dawa katika kitongoji cha Kilulumo, kijiji cha Itagata Tarafa ya Itigi wilayani Manyoni.

Alisema tukio lilitokea kitongoji cha Lulanga kijijini hapo Januari 25, mwaka huu saa 9.30 alasiri wakati mjamzito huyo akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Misheni ya Itigi kwa matibabu zaidi kutokana na kuvuja damu nyingi baada ya kujifungulia kwenye duka la Dawa la Hengwe.

Alisema kuwa siku moja kabla, mume wa mjamzito huyo alimpeleka mkewe kwenye Zahanati ya kijiji Itagata ili kufanyiwa uchunguzi ambapo inadaiwa muuguzi wa Zahanati hiyo, Grace Simon iliwaambia njia ya uzazi ilikuwa haijafunguka; hivyo akawashauri warudi nyumbani.

Alisema kuwa aliporejea nyumbani hali ya mjamzito huyo ikawa mbaya hivyo kumlazimu mumewe kumpeleka Zahanati ya jirani ya Misheni katika Kijiji cha Mitundu kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo, Kamanda Magiligimba alidai kuwa wakiwa njiani, mumewe aliona hali ya mkewe inazidi kuwa mbaya zaidi, aliamua kumpeleka kwenye duka la dawa muhimu linalomilikiwa na Hengwe lililopo jirani ambapo alijifungua mtoto wa kiume.

“Kutokana na mjamzito huyo kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua, mumewe aliamua kumkimbiza katika Hospitali ya Misheni ya Itigi kwa pikipiki lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kufika mbali kabla ya mama huyo kufariki dunia,” alisema Magiligimba.

Download  Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment