Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura (kushoto) pamoja na Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif (kulia) wakiwa kwenye baadhi ya madawati yaliyochangiwa na kampuni hiyo ikiwa ni jitihada za kuunga mkono kampeni ya kuchangia madawati nchi nzima iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli. Zoezi hio la uchangiaji wa madawati lilifanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mtwara mwishoni mwa wiki hii.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura (kushoto) pamoja na Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif (kulia) wakiwa wamekaa kwenye madawati hayo.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura (kulia) , akizungumza wakati wa kupokea madawati hayo. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mh. Dkt. Khatib Malimi Kazungu
Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif (kushoto), akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo.
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi.
Anastazia Wambura amepokea madawati hamsini yenye thamani ya shilingi
milioni tano kutoka kwa kampuni ya matangazo ya dijitali ya StarTimes
ikiwa ni jitihada za kuunga mkono kampeni ya kuchangia madawati
iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John
Pombe Magufuli.
Akizungumza mara baada ya hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika
mwishoni mwa wiki moani Mtwara, Mh. Bi. Wambura amebainisha kuwa zoezi
la kuchangia madawati ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira
mazuri linawahusu watu wote na sio serikali pekee.
“Ningependa kuchukua fursa hii kuzipongeza taasisi za umma na sekta
binafsi kwa mwitikio wao mkubwa wa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais
katika kampeni ya kuchangia madawati.
Wote tunafahamu ni kwa kiasi gani
shule nyingi nchini zinavyokabiliwa na uhaba wa madawati jambo
linalopelekea mazingira magumu ya kufundishia na kujinzia. Lakini kwangu
mimi suala la wanafunzi kuongezeka sioni kama ni tatizo bali ni
changamoto kwa serikali yetu na jamii kwa ujumla kuendana na mwamko
mkubwa wa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule. Kwa muda mrefu
sana serikali imekuwa ikiwahamasisha wananchi wake wawapeleke watoto
shule na wakafanya hivyo, sasa suala hilo tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa
na vivyo jinsi walivyoitikia mwamko huo basi waitikie na wa huu wa
kuchangia madawati.” Alisema Mh. Bi. Wambura
Naibu Waziri huyo aliendelea kwa kuelezea kuwa serikali ina wajibu
wa kuhamasisha maendelea kwa wananchi wake kwa njia mbalimbali ikiwemo
hii ya kuwasilisha maeneo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele kama vile
suala la elimu nchini.
“Elimu ndio suala la msingi katika taifa lolote duniani iwe
lililoendelea au linaloendelea na ndio maana kwa nchi za wenzetu
wanawekeza fedha nyingi katika sekta hii. Nchi yoyote yenye wasomi wengi
lazima itakuwa na maendeleo makubwa kutokana na raia wake kuelimika
lakini hayo yote haya hayatowezekana kama tusipowawekea mazingira mazuri
wanafunzi wetu tangu ngazi ya msingi,” alisema Mh. Naibu Waziri na
kumalizia, “Ningependa kumalizia kwa kuwapongeza na kuwashukuru wenzetu
wa kampuni ya StarTimes kwa kuguswa na suala hili na kuamua kuja huku
Mtwara kuchangia madawati kwani huku ndiko kwenye changamoto kubwa hasa
kutokana na taasisi na makampuni mengi kuwepo sehemu za mijini.
Tunawashukuru sana na tunawaomba muendelee na moyo huo huo na mfike
sehemu nyingine amabko makampuni mengine hayafiki.”
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura
Hanif amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ni mdau mkubwa wa masuala ya
kijamii hususani elimu kwa inafahamu umuhimu wake katika kuleta
mapinduzi ya kimaendeleo.
“StarTimes ni mdau mkubwa sana wa masuala ya elimu na kwa muda
mrefu tumekuwa tukisaidia shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Uchangiaji wa madawati ni kampeni ya aina yake iliyoanzishwa na Mh. Rais
Magufuli na inahitaji kuungwa mkono kwa nguvu zote kwani yeye aliamini
kabisa watanzania tunao uwezo huo ila tulikosa tu uhamasishaji. Na ni
kweli uhamasishaji ndio uliokosekana kwani mara baada ya kutoa tamko
hilo taasisi, makampuni, mashirikia, wananchi na watu binafsi
wameonyesha mwitikio mkubwa. Hii ni dalili njema kwamba watanzania
tunaweza kuleta maendeleo yetu wenyewe bila ya kungojea msaada kutoka
kwa watu wa nje.” Alisema Bi. Hanif
“Leo hii tumekuja huku Mtwara kuja kukabidhi madawati haya,
tunafahamu kwamba ni machache lakini yatakuwa ni msaada mkubwa kwa
watoto wetu kusoma katika mazingira mazuri. Wanafunzi wanaposoma katika
mazingira mazuri hupelekea kuhudhuria vipindi, kuipenda shule, kuelewa
vizuri na hatimaye kupelekea kufaulu masomo yao,” alisema na kuhitimisha
Bi. Hanif kuwa, “Wananfunzi wanapowekewa mazingira mazuri ya kusomea
pia hutoa hamasa kwa walimu kufanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa kwani
ufundishaji unakuwa ni rahisi na vivyo hivyo uelewa kwa wanafunzi. Hivyo
basi, ningependa kutoa wito kwa wanafunzi wayatunze madawati haya ili
yaje kuwanufaisha na wenzao watakaokuja siku za usoni na tunawaahidi
kuwa tuko pamoja nao katika kutatua changamoto zinazowakabili.”
0 comments:
Post a Comment