MATABIBU wanne wa Tiba Asilia na Mbadala akiwemo mmiliki wa Kliniki ya Sure Herbal, Simon Rusigwa wamewasilisha maombi ya kuomba ruhusa ya kufungua kesi ya kupinga uamuzi wa kufutiwa leseni za kutoa huduma za kitabibu.
Wamewasilisha
maombi hayo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam,
dhidi ya Baraza la Tiba Asilia na Mbadala, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Mbali
na Rusigwa, matabibu wengine waliowasilisha maombi hayo kupitia kwa
Wakili Dk Lucas Kamanija, ni Abdallah Mandai wa kliniki ya Mandai
Herbalist, Fadhili Kabujanja wa Fadhaget Sanitarium na John Lupimo wa
Lupimo Sanitarium.
Maombi
hayo yalitakiwa kusikilizwa jana mbele ya Jaji Ama–Isario Munisi wa
mahakama hiyo, hata hivyo kabla ya kuanza kusikilizwa, Serikali
iliwasilisha pingamizi la awali ikidai kuwa maombi hayo hayakufuata
misingi ya kisheria.
Katika
pingamizi hilo serikali inadai kuwa maombi hayo yana kasoro kwa kuwa
waombaji hawajapita njia zote zinazotakiwa wazifuate ndipo waende
mahakamani pia wanadai maombi hayana miguu ya kusimamia kwa kuwa hati ya
viapo vya walalamikaji vina upungufu ya kisheria.
Baada
ya kuwasilishwa kwa pingamizi, Jaji Munisi aliahirisha shauri hilo hadi
kesho saa 8 mchana, ambapo alizitaka pande zote zinazohusika ziwepo ili
kusikiliza pingamizi hilo.
Katika
maombi yao, matatibu hao wanadai, wameamua kupeleka maombi hayo
mahakamani, kwa kuwa wanaamini walifutiwa leseni bila kufuata taratibu
za kisheria.
Wamedai
wanaamini uamuzi uliochukuliwa umetolewa bila kupitia Kamati ya Maadili
ya Baraza la Tiba Asilia na Mbadala, huku wakidai kuwa huo si uamuzi
bali zilikuwa tuhuma mpya, lakini hawakupewa nafasi ya kusikilizwa.
0 comments:
Post a Comment