Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa siku 14 kwa Bodi ya Wakurugenzi wa
Taasisi ya Mifupa (MOI) kuangalia matatizo yaliyopo na kuyafanyia
tathmini, huku akisisitiza kambi za upasuaji zirejee na zianze kazi mara
moja ifikapo Agosti 13, mwaka huu.
Alisema bodi hiyo itakapokaa
na kurudisha majibu kwake atafanya maamuzi likiwamo suala la uteuzi wa
mkurugenzi wa taasisi hiyo, akisema imekaimiwa kwa kipindi kirefu na
sasa ni wakati wa kumpata wa kuishikilia.
“Kitu kinachonisumbua
kichwa kwa sasa ni kuhusiana na kambi za upasuaji, naomba zianze kazi
mara moja, wanaoteseka ni wananchi wa hali ya chini maana baada ya
kufutwa kambi za upasuaji ikaanzishwa kambi ya upasuaji wa watu
wanaolipia, wasiojiweza wanahudumiwa vipi?” alihoji.
Kauli ya
Ummy imekuja baada ya kikao cha ndani alichokifanya jana na wafanyakazi
wa taasisi hiyo, ambao walitoa malalamiko mbalimbali kuhusu utendaji wa
taasisi, stahiki zao pamoja na malalamiko mengine waliyoyaandika kwenye
makaratasi na kuwasilisha kwake.
“Baada ya kuwaambia muandike
kwenye vikaratasi, nimegundua kwamba mlishindwa kusema wazi ila molari
ya wafanyakazi ipo chini na baada ya kusoma kwa makini nimegundua hakuna
ushirikiano wa kutosha,” alisema Ummy.
Ummy alisema katika
kutatua changamoto kadhaa ndani ya taasisi ataanza kwa kupeleka CT Scan
mpya, lakini pia bajeti ya vifaa tiba kiasi cha Sh3 bilioni.
Aliunga
mkono wazo la madaktari wa taasisi hiyo ambao
walimtaka kupeleka muswada bungeni wa kupitisha sheria ya malipo ya
kuchangia huduma katika mfuko wa Trauma Fund kwa watu wote wanaotumia
vyombo vya usafiri ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaopata ajali.
“Naunga
mkono hoja hii, lakini siwezi kuisemea moja kwa moja mpaka ipate baraka
kutoka Baraza la Mawaziri, maana ninachokitaka ni kusaidia maskini
wasiojiweza ambao ndiyo hao kila siku wanagongwa na pikipiki na magari,
ndiyo wahanga wa hizi ajali,” alisema Ummy.
Akizungumza kwa msisitizo, Ummy alisema lengo lake kubwa ni kuhakikisha
sekta ya afya inakuwa bora kwa kipindi chake atakachokuwa waziri wa
afya huku akiahidi kushughulikia kero mbalimbali za wafanyakazi
walizoziwasilisha kwake.
Akizungumza awali Kaimu Mkurugenzi wa
Taasisi ya Mifupa (MOI) Dk Othman Kiloloma alisema wanakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo motisha na posho kwa wafanyakazi.
Alisema
deni la MOI limekuwa sababu ya Taasisi kukosa vifaa na vitendanishi kwa
wakati kutokana na wasambazaji wengi kushindwa kuhudumia.
Dk
Kiloloma alisema mwaka 2014 wakati anapokea Taasisi hiyo kama Kaimu
Mkurugenzi alikutana na deni kubwa la stahiki za wafanyakazi kiasi cha
Sh4 bilioni pamoja na deni upande wa Saccos kiasi cha Sh500 milioni na
kwa sasa wamefanikiwa kulipia Sh600 milioni.
Alisema jengo jipya
la MOI bado linahitaji kiasi cha Sh20.6 bilioni ili kukamilisha vifaa
vinavyohitajika ikiwemo samani muhimu.
“Tatizo kubwa
tunalopambana nalo hivi sasa ni jengo jipya la MOI, ambalo bado
hatujakabidhiwa mpaka sasa, kwanza lina upungufu mkubwa ikiwemo lifti
kutokufanya kazi, jengo zima ili likamilike linahitaji kiasi cha Sh8.6
bilioni,”alisema Dk Kiloloma.
Wafanyakazi wafunguka
Wakitoa
malalamiko yao kwa Waziri, wafanyakazi hao walizungumzia mambo makubwa
manne likiwemo la stahiki ya mishahara yao na malipo, uchakavu wa vifaa
tiba, maendeleo ya rasilimali watu na mrundikano wa wagonjwa.
Pamoja
na mambo mengine wafanyakazi
hao walilalamikia suala la kutopandishwa vyeo, kutopanda kwa mishahara
na malipo ya ziada kuwa hayatoshelezi, huku wengine wakifanya kazi kwa
miezi sita bila malipo.
Mmoja wa wauguzi wa MOI, Mwajabu Ali
alisema vitanda vilivyopelekwa na Rais John Magufuli baada ya kuzuiwa
kwa mchapalo, vimekuwa na upungufu mkubwa ikiwemo kukosa matairi, jambo
ambalo linaleta ugumu wa utoaji wa huduma.
Alisema jengo hilo
jipya limekuwa na matatizo ya lifti, hivyo inakuwa kazi kubwa
kumsafirisha mgonjwa kutoka wodini mpaka kumfikisha katika chumba cha
upasuaji au kipimo.
“Tunafanya kazi katika mazingira magumu,
vitanda havina matairi, lifti mbovu, hakuna maji, oksijeni za ukutani
hakuna, tunatumia mitungi ambayo hata hivyo ni mizito sana kuibeba,”alisema Mwajuma.
Kaimu Mkurugenizi wa MOI Dkt. Othman Kiloloma akizungumza mbele ya watumishi wa Taasisi ya mifupa muhimbili (MOI) hawapo pichani kabla ya kumkaribisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu hayupo pichani wakati alipokwenda kusikiliza changamoto za watumishi hao jijini Dar es salaam.
0 comments:
Post a Comment