MAMLAKA
ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) imevipa onyo na kuvipiga
faini vituo viwili vya televisheni na kimoja cha redio kwa kukiuka
maadili ya utangazaji.
Vituo
hivyo ni ITV, Clouds Tv na Clouds Fm Radio, vyote vya jijini Dar es
Salaam, ambavyo kwa ujumla vimepigwa faini ya Sh milioni 19.
Akitoa
uamuzi uliofikiwa na Kamati ya Maudhui ya TCRA, Makamu Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Joseph Mapunda alisema vituo hivyo vilibainika kukiuka
Kanuni za Huduma za Utangazaji na kuvitaka kuwa wasimamizi wazuri wa
vipindi vyao.
Mapunda
alisema kamati hiyo imekipa onyo na kukipiga faini ya Sh milioni 10
kituo cha televisheni cha ITV kwa makosa mawili; la kwanza ni kupitia
kipindi chake cha Kumekucha cha Juni 15, mwaka huu kati ya saa 1:00 na
1:30 asubuhi ambacho mtangazaji alifanya mahojiano na Mbunge wa Iringa
Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kuhusu mwenendo wa Bunge la Bajeti, na
Mchungaji Msigwa alitamka maneno ya kashfa dhidi ya Naibu Spika wa
Bunge, Dk Tulia Ackson.
“…mtangazaji
hakuchukua jitihada za kumwomba Mheshimiwa Peter Msigwa kufuta lugha ya
matusi aliyoitumia, bali alionekana akifurahia na kuendelea kumuuliza
maswali mengine,” alisema Mapunda.
Katika
kosa la pili, Mapunda alisema kituo hicho kilikiuka kanuni katika
taarifa ya habari ya Juni 23 kati ya saa 1:00 na 2:00 asubuhi,
kilitangaza taarifa ya msichana wa miaka 16 aliyebakwa na kupewa
ujauzito na walitumia utambulisho wa msichana huyo kwa jina na shule
anayosoma.
Katika
utetezi wake, Mwakilishi wa ITV, Stephen Chuwa alikiri kuwa Mchungaji
Msigwa alitoa maneno ya kashfa na hakutembea katika ahadi yake ya
kutomkashifu mtu.
Aidha
alisema kama mtangazaji angemuomba kufuta kauli, mjadala ungekuwa
mkubwa zaidi. Alisema watachukua hatua za kumwomba radhi Dk Tulia
kutokana na kashfa hiyo.
Kwa
upande wa Kituo cha Clouds Tv, kituo hicho kimepewa onyo na kupigwa
faini ya Sh milioni nne ambazo wanapaswa kulipa ndani ya siku 30 kuanzia
siku ya hukumu.
Mapunda
alisema kituo hicho kupitia kipindi chake cha Hip Hop, kilichorushwa
kati ya saa 8:00 mchana na 12:00 jioni, kilirusha video ya nyimbo za
Asanteni kwa Kuja wa Mwana FA na Break It Down wa Lil Bebbie, ambazo
zinadhalilisha utu wa mwanamke.
Aidha,
Clouds Fm pia imepewa onyo na kupigwa faini ya Sh milioni tano kwa
vipindi vyake vya ‘Power Breakfast’ na Jahazi kwa walikiuka kanuni za
utangazaji.
Alisema
katika kipindi cha Jahazi cha Mei 9, kilichorushwa kati ya saa 10:00
hadi 12:55 jioni, watangazaji walisikika wakishabikia taarifa ya mtu
kufanya ngono na mbuzi, ambako walieleza kuwa mtu huyo na mbuzi ni kama
mtu na mpenzi wake, jambo lililoonesha wanahamasisha vitendo hivyo.
Aidha,
Mei 18, mwaka huu katika kipindi cha Power Breakfast, kilichorushwa
kati ya sa 12:00 na 4:00 asubuhi baada ya kusoma taarifa ya Hospitali ya
Taifa Muhimbili kuhusu kupandikizwa kwa sehemu za siri za kiume kwa
mtoto wa miaka mitatu, aliyezaliwa akiwa hana na kulelewa kama mtoto wa
kike.
0 comments:
Post a Comment