Serikali imesema kuwa itaendelea kuboresha maslahi ya askari wa Jeshi la Polisi na kuwajengea nyumba za kisasa za kuishi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
Mhe. Luhaga Mpina wakati akijibu maswali ya wabunge kuhusu mkakati wa
Serikali wa kuboresha maslahi ya Askari wa Jeshi hilo kwa niaba ya Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Bungeni mjini Dodoma leo
Amesema
kuwa Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 itatekeleza Mpango
kabambe wa ujenzi wa nyumba za Polisi 4136 ambao utakwenda sambamba na
ujenzi wa vituo vya Polisi.
Amesema
Serikali imechukua hatua za haraka kulishughulikia suala la ukosefu wa
nyumba za askari hao katika maeneo mbalimbali nchini ili kuimarisha
ulinzi na usalama katika maeneo yenye ukosefu wa nyumba hizo.
Amelieleza
Bunge kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha
kuwa maslahi ya Askari Polisi yanaimarishwa ikiwemo malipo ya Posho ya
pango kwa askari wasio na nyumba ambayo ni asilimia 15 ya mishahara yao
ili waweze kulipia gharama hizo.
Ameongeza
kuwa askari wenye utalaam maalum wakiwemo madereva na madaktari
wamekuwa wakilipwa posho ya asilimia 15 ya mishahara yao na kuongeza
kuwa askari wanaoajiriwa katika ajira mpya kama madaktari wamekuwa
wakilipwa mishahara sawa na madaktari wengine bila kujali vyeo vyao.
“Serikali
tumefanya jitihada kubwa sana kuboresha maslahi ya askari wetu, kama
Serikali tumetoa posho za nyumba, posho za utalaam maalum kwa askari
wote ambayo ni asilimia 15 ya mshahara wa kila Polisi hii yote ni
kuwafanya askari wetu waweze kumudu gharama za maisha” Amesisitiza Mhe. Mpina.
Ameeleza
kuwa kwa askari wanaofanya kazi katika mazingira magumu wakiwemo wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wamekuwa wakipewa posho ya kufanya kazi
katika mazingira magumu (Hardship allowance) kiasi cha shilingi laki
moja (100,000) kila mwezi.
Mhe.
Mpina amebainisha kuwa askari wote wanaohitimu mafunzo yao wamekuwa
wakikatiwa Bima ya Afya kwa asilimia 100 na Serikali pamoja na udhamini
wa mikopo mbalimbali katika taasisi za kifedha ili waweze kupewa mikopo
na taasisi hizo.
Aidha,
amesisitiza kuwa serikali imewapandishia kiwango cha Posho ya katikati
ya mwezi (Ration Allowance) kutoka shilingi 180,000 za awali hadi
300,000 ambazo wanalipwa kwa sasa nchi nzima.
Katika
hatua nyingine Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imetoa
ufafanuzi kuhusu vijana wa kidato cha nne kutochukuliwa kujiunga na
Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa
hatua ya kuwachukua vijana wote wanaomaliza kidato cha nne kwa sasa
haiwezekani kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Serikali.
Amesema
kuwa uwezo wa JKT kuchukua vijana wa kujitolea kwa sasa ni 5000 hadi
7000 kwa mwaka kulingana na bajeti inayotolewa na kuongeza kuwa mpango
wa Serikali ni kuendelea kutenga fedha na kujenga kambi zaidi za mafunzo
ili kuwawezesha vijana wengi kujiunga na mafunzo hayo kulingana na
upatikanaji wa fedha.
Kwa
upande wa wahitimu wa kidato cha sita wanaotakiwa kujiunga na JKT kwa
mujibu wa Sheria Mhe. Mwinyi amesema Serikali imewachukua vijana 14,000
na inaendelea kujenga uwezo wa ndani wa kuchukua vijana wengi zaidi.
Amesema
Serikali inakusudia kujenga majengo ndani ya makambi ili kuwezesha
vijana wote wanaohitimu kidato cha sita kupitia JKT kabla ya kujiunga na
vyuo mbalimbali hapa nchini.
Aidha,
Amefafanua kuwa kwa wale wanaojiunga na JKT kwa kujitolea ambao idadi
yao inafikia 5000 sio wote wanaopata nafasi ya kuajiriwa katika vyombo
vya Ulinzi na Usalama na kuongeza kuwa ni asilimia 71 ndio hupata ajira
kwenye vyombo hivyo huku waliobaki wakilazimika kurudi nyumbani.
Amebainisha
kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaangalia utaratibu wa
kuwawezesha vijana hao ili wanaporudi uraiani waweze kupatiwa mitaji ya
kuwawezesha kujiajiri wenyewe.
0 comments:
Post a Comment