Jeshi
la polisi mkoani Dodoma, linawashikilia askari watatu wa wanyamapori wa
pori la akiba Swagaswaga wilayani Kondoa, wakituhumiwa kumuua mkazi wa
kijiji cha Olimba wilaya ya Chemba kwa kumpiga risasi mgongoni
wakimtuhumu kubeba nyama pori.
Akizungumza
ofisini kwake leo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Lazaro Mambosasa,
alisema tukio hilo lilitokea Disemba 31,mwaka jana saa 7:30 mchana
katika kijiji cha Selya kata ya Selya wilayani humo.
“Marehemu
ambaye hakufahamika jina lake lakini mkazi wa kijiji hicho, alikuwa
akiendesha pikipiki huku akiwa amepakia kiroba kilichokuwa na sukari
guru ndani yake, lakini askari wanyamapori hao walimhisi amebeba nyama
pori na bila kumsimamisha na kumhoji waliamua kutumia bunduki zao kumuua
papo hapo,” alisema Kamanda Mambosasa.
Aidha
Kamanda huyo amesema baada ya kufanya mauaji hayo, askari hao waliubeba
mwili huo kwenye gari walilokuwa nalo pamoja na pikipiki ya marehemu na
kiroba cha sukari guru, kisha kwenda kuutelekeza mwili huo ndani ya
pori hilo la Swagaswaga.
“Baada
ya kuutelekeza mwili huo ndani ya pori hilo, walichukua pia pikipiki na
kiroba na kuvificha kila kimoja mahali pake kwa lengo la kupoteza
ushahidi wa tukio hilo”.
Kamanda
Mambosasa alisema wakati askari hao wanafanya tukio hilo, walishuhudiwa
na mwananchi mmoja wa kijiji hicho ambaye alijificha porini ambaye
aliamua kutoa taarifa kituo cha polisi Kondoa.
Wahusika
wa tukio hilo ambao wanaendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa
mahakamani ni George Grefee (26), Chini Paulo (40) na Christopher Waunko
(36).
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment