Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) jana alikana tuhuma za makosa
ya jinai kwa pamoja na mkewe, Neema, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Arusha.
Mbele
ya Hakimu Mkazi, Nestory Barro, Lema na Neema walikana mashtaka ya
kutuma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi wenye matusi kwa Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mrisho Gambo.
Awali
akiwasomea maelezo ya kesi hiyo Wakili wa Serikali Alice Mtenga alidai
kuwa Lema na Neema, Agosti 20 mwaka jana, ndani ya Jiji la Arusha,
walimtumia ujumbe wa simu ya kiganjani kwa mkuu huyo wenye lugha ya
matusi, huku wakijua ni kosa kisheria.
Ilidaiwa
kuwa ujumbe huo ulitumwa kutoka simu namba 0764-150747 kwenda namba
0766-757575 uliokuwa ukidai, “Karibu, tutakudhibiti kama Uarabuni
wanavyodhibiti mashoga.”
Baada
ya kuwasomea maelezo hayo ya awali, washtakiwa hao kwa pamoja walikiri
kuwa ni wakazi wa Arusha na Lema ni Mbunge wa Arusha Mjini ila walikataa
kusambaza ujumbe huo wa kumtukana Gambo na tarehe ya kukamatwa kwao.
Hakimu
Barro aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 3, ambapo upande wa Jamhuri
utaanza kuwasilisha ushahidi wake Gambo akiwa wa kwanza.
Baada
ya kesi hiyo kuahirishwa, wakili wa Lema, John Mallya aliiambia
mahakama wanatoa notisi ya kuwasilisha pingamizi la mdomo kwa kuwa hati
ya mashtaka ina mapungufu, na baadaye wataomba mahakama iitupilie mbali
hati hiyo.
Hata hivyo, Hakimu huyo alisema hoja za awali za pingamizi hilo zitasikilizwa Februari 3 pia.
Mbali na Mkuu wa Mkoa, Jamhuri inakusudia kuita mashahidi wengine wanne, ilielezwa.
Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Mtenga upande wake pia utakuwa na vielelezo vitatu vitakavyotolewa
mahakamani hapo.
Alisema
mashahidi watano watakaotoa ushahidi wao ni Gambo, Mkuu wa Upelelezi
Mkoa wa Arusha (RCO), George Katabazi, (ASP) Damasi Massawe, mhusika
kutoka kampuni ya simu ya Vodacom pamoja na mtaalamu wa picha.
Pia
alivitaja vielelezo watakavyovitoa katika kesi hiyo kuwa ni nakala ya
taarifa za mawasiliano ya simu kutoka kampuni ya Vodacom, simu ya
mshtakiwa mke wa Lema na taarifa ya uchunguzi kutoka kitengo
kinachoshughulikia masuala ya kiuchunguzi (Forensic Bureau).
Wakati
huo huo, wakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, John Mallya
amemuomba Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Bernard Nganga
kutoanza kusikiliza kesi ya kuhamasisha maandamano Septemba Mosi (Ukuta)
inayomkabili Lema peke yake.
Akitoa
ombi hilo jana, Mallya alidai kuwa kesi hiyo ya kuhamasisha maandamano
kwa njia ya mtandao wa kijamii kisha kuusambaza Agosti Mosi hadi Agosti
26 mwaka jana, haifai kusikilizwa katika mahakama hiyo sababu kuna hoja
za Kikatiba.
Alisema
shahidi aliyeandaliwa kwa ajili ya kutoa ushahidi wake ambaye ni RCO,
George Katabazi hapaswi kutoa ushahidi mahakamani hapo, sababu kesi hiyo
ina hoja za kikatiba.
“Mheshimiwa
kesi hii ukiiangalia ipo kikatiba zaidi na kwasababu ipo kikatiba basi
sisi tunaenda Mahakama Kuu ikasikilizwe na majaji watatu ili tupewe
tafsiri ya vifungu vya sheria," alisema Mallya.
Alisema kwa Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977 inampa haki kiongozi au mwanasiasa kufanya shughuli za kisiasa.
"Kuwakataza au kuingilia kati tunataka kujua huko Mahakama Kuu ya Katiba, nani ana mamlaka ya kuzuia maandamano."
Naye
wakili wa Serikali Mtenga alimuomba hakimu kutupa pingamizi la Mallya
alilolitoa mahakamani hapo, badala yake kesi hiyo iendelee kusikilizwa
kwani upande wa Jamhuri tayari ulishamuandaa
shahidi wake.
Hakimu Nganga alisema amesikia hoja za mawakili hao wa pande zote mbili na yeye anaendelea na kesi hiyo baada ya aliyekuwa
Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Augutino Rwezile kupanda
cheo na kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kitengo cha biashara.
Alisema atatoa uamuzi wa kesi hiyo, kusikilizwa au kwenda kwa majaji watatu Februari 8.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
0 comments:
Post a Comment