Wednesday 29 March 2017

Exclusive..Nay wa Mitego Afunguka Mazito kwa Saa 36 Alizokuwa Chini ya Ulinzi wa Polisi,Afunguka Mengi ya Kushangaza Aliyofanyiwa na Polisi.Fahamu zaidi hapa.

Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuamuru msanii wa muziki wa kizazi kipya, Emmanuel Elibariki maarufu ‘Ney wa Mitego’ kuachiwa huru na baadaye kusema ameitwa Ikulu, rapa huyo amefunguka na kueleza kilichojiri katika saa 36 alizokuwa chini ya ulinzi wa polisi.
Ney wa Mitego alikamatwa Machi 26 alfajiri huko Turiani mkoani Morogoro, akikabiliwa na tuhuma za kusambaza wimbo wenye maudhui ya kuitukana Serikali. Hata hivyo, aliachiwa huru juzi alasiri katika Kituo cha Kati jijini Dar es Salaam.
Saa chache baada ya kuachiwa huru juzi, taarifa za Ney kuitwa Ikulu zilienea na kuthibitishwa na msanii huyo jana.
Pia, alihojiwa na kituo cha Televisheni cha Azam ambako alikiri kupata mwaliko wa kwenda Ikulu kesho kutwa kwa ajili ya mazungumzo na Rais Magufuli.
“Ni kweli kuna taarifa kama hizo, ila siwezi kuzungumza sana kwa sasa kwa kuwa masuala haya yapo chini ya sheria,”alisema.
Afunguka saa 35 alizoshikiliwa
Akisimulia tangu alivyokamatwa saa 10 alfajiri ya Jumapili hadi alipoachiwa Jumatatu ya Machi 27, Ney alisema alifuatwa na polisi katika hoteli ya Premier Lodge mara baada ya kumaliza shoo aliyokuwa akiifanya huko Turiani.
“Asubuhi nikapelekwa Kituo cha Dakawa, Mvomero huko nilikaa kwa saa chache kisha wakanipeleka kituo kikuu cha Morogoro mjini. Nilichoambiwa huko ni kwamba ninatakiwa kujibu tuhuma za kesi ya matusi kuhusu wimbo wangu mpya ‘Wapo’,” Alisema.
Alisema baada ya kukaa mahabusu kwa saa kadhaa walifika askari kutoka Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam na kumchukua akiongozana na polisi kutoka Morogoro saa nane mchana, tayari kwa safari ya Dar es Salaam.
“Jioni tulifika na hapa nilipokelewa na kuingizwa tena mahabusu, huko nilikaa na nikalala bila kuambiwa chochote,” alisema.
Hata hivyo, alisema alishangazwa na namna askari walivyokuwa wakiendesha shtaka lake, kwani hawakutaka kumuuliza chochote hata siku ya pili ndugu zake walipofika kumuulizia waliambiwa hayupo.
‘Mpaka sasa sijui ni kwanini ndugu, watu wa karibu na jamaa walipokuwa wakija kuniulizia waliambiwa sijafikishwa kituoni hapo, wakati huo wote mimi nipo mahabusu hapa Dar” alisema.
Alisema hata polisi walipoanza kumuhoji, walimuhoji kwa makosa ya mtandaoni huku wakidai kosa kubwa ni wimbo ulioikashfu Serikali.
Hata hivyo, alisema muda huo wote hakukuwa na Ofisa yeyote wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
“Nilihojiwa kwa takribani saa mbili na nusu hivi, wakati huo wote nilikuwa na maofisa upelelezi wawili pekee na baadaye nilirudishwa mahabusu,” alisema.
Licha ya mikiki hiyo yote, Ney alisema mpaka anaondoka Kituo cha Kati hakuambiwa kwa nini aliruhusiwa:
“Haya ni masuala ya kisheria zaidi hivyo siwezi kuhoji sana niliondoka baada ya wao kunishikilia kwa saa 30 na zaidi” alisema
Kuhusu kuboresha ‘Wapo’
Kuhusu kuboresha wimbo wake kama alivyoambiwa na Rais, Ney wa Mitego alisema amepokea maoni hayo na kwamba yupo katika mchakato wa kuuboresha na kuahidi hatavuka mipaka.
“Ninalifanyia kazi mheshimiwa amesema anaupenda wimbo wangu na anausikiliza, yeye mwenyewe amewekwa kwenye huu wimbo ni jambo ambalo hawezi kupuuzia na hiki kinachoendelea labda amefurahishwa, hivyo nitaifanyia kazi kwa kuongeza mengi makubwa na kwa mapana zaidi bila kuvuka mipaka,” alisema.
Alisisitiza kuwa yeye ni mwanamuziki na si mwanasiasa, hivyo kwa yeyote akitaka kumhukumu anatakiwa amhukumu kama mwanamuziki.
“Naona Rais ni mwelewa, tukimwambia tunahitaji nini atatuelewa ingawa inatakiwa tusivuke mipaka na wananchi pia wanatakiwa kuzungumza vikiwemo vyombo vya habari,” alisema.


Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment