Uamuzi huo umechukuliwa baada ya watu wanane kuuawa kinyama kwa kuchinjwa juzi usiku katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, Manispaa ya Tanga.
Habari
za uhakika ambazo tulizipata jana, zinasema tayari vikosi hivyo
vimeanza operesheni kali katika mapango ya Amboni ambayo yanadaiwa kuwa
maficho ya watu hao.
Akitoa
salamu za rambirambi wakati wa mazishi ya marehemu wanne kati ya wanane
waliozikwa Kibatini jana, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,
Jenerali Davis Mwamunyange, alisema vyombo vya dola vitahakikisha watu
wote waliohusika katika mauaji hayo wanatiwa mbaroni.
“Ndugu
zangu nawapeni pole kutokana na kuondokewa na wapendwa wetu… naomba
kuwahakikisha sisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola
tutahakikisha tunawatia nguvuni watu wote waliohusika na mauaji haya,” alisema Jenerali Mwamunyange.
Alisema tukio la mauaji hayo ni la kusikitisha mno kutokana na Tanzania kusifika kuwa nchi ya amani duniani.
“Tanzania inasifika kuwa na amani duniani kote, lazima hatua za kiusalama zichukuliwe haraka ili kunusuru amani yetu isichezewe.
“Ni tukio la ajabu ambalo limegusa watu wengi wasio na hatia, tutasaidiana na wenzetu kuhakikisha wahalifu hawa wanapatikana,” alisema Jenerali Mwamunyange.
Naye
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni Hamad Masauni, alisema
Serikali inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo ili kuwakamata
wahusika ndani ya kipindi kifupi.
Aliwahakikisha wananchi kuwa ulinzi unaimarishwa na kwamba matukio hayo hayatajirudia tena.
“Vyombo vya ulinzi vitafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha tunawatia nguvuni haraka watu waliohusika na mauaji hayo,” alisema Masauni.
Aliwaomba ndugu na jamaa ambao wamefiwa na ndugu zao kuwa na subira wakati Serikali inaendelea kuchukua hatua.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu alisema wataendelea kuimarisha ulinzi na usalama maeneo yote.
Katika
hatua nyingine, wakazi wa mitaa mitatu ya Mleni Kati, Mleni Mashariki
na Kibatini katika Kata ya Mzizima, Manispaa ya Tanga, wameanza kukimbia
makazi yao kwa kuhofia usalama wao baada ya mauaji hayo.
Mauaji
hayo yalitokea juzi usiku ambapo watu wanaoaminika kuwa majambazi
walivamia nyumba tatu katika eneo hilo, wakiwa wamelala usiku, kisha
kuwateka na kuwapeleka msituni kabla ya kuwachinja.
Wakazi
hao wanaounda zaidi ya kaya 30, walisema wameamua kuyakimbia makazi yao
kwa kutokuwa na imani ya usalama wao katika eneo hilo, baada ya wale
wanaoitwa majamabzi kuvamia makazi yao kwa mara ya pili kwa staili ya
kutisha.
Kabla
ya tukio hilo la juzi, watu wasiofahamika walivamia makazi yao na
kuchinja kuku 40, mbuzi wanne na ng’ombe mmoja na kukimbilia mapango ya
Amboni na hawajawahi kukamatwa.
Mwandishi
wetu jana alishuhudia wanawake na watoto wakiwa na mizigo mithili ya
wakimbizi wakiondoka katika eneo hilo huku wanaume wakibaki kwa ajili ya
kuzika ndugu, jamaa na marafiki zao waliouawa katika tukio hilo.
Mmoja
wa wananchi hao, Juma Issa, alisema wamelazimika kuwahamisha wanawake
na watoto kwa kuhofia wanaweza kuvamiwa tena kwa mara ya pili.
Nae
Lucas Muhina alisema kuwa anashindwa kuhama katika eneo hilo kutokana
na kuwa na mifugo, hivyo anashindwa kujua mahali salama pa kuihifadhi.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kibatini, Shabani Mwamini, alithibitisha baadhi ya wananchi wa mitaa mitatu kuhama katika eneo hilo.
“Nyumba nyingi zimebaki na wanaume pekee yake kwani wanawake na watoto wote wamehama kwa sasa,” alisema.
Wakati huohuo, maiti nne kati ya nane zimezikwa jana huku nyingine nne zikisafirishwa nje ya mkoa huo.
Mwamini aliwataja waliozikwa kuwa ni Issa Husein, Mkola Husein, Issa Hamis na Salim Adam.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella alisema kuwa vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Simulizi ya Mauaji
Mtoto
wa marehemu Mkola Hussein anayeitwa Salimu Mkola (16) alisababisha
vilio na simanzi kwa waombolezaji baada ya kusimulia namna watu hao
walivyomchukua baba yake na kwenda kumchinja mbele ya nyumba yake.
Akisimulia
tukio hilo huku akibubujikwa machozi, mtoto huyo alisema watu hao
walifika nyumbani kwao wakagonga mlango saa sita usiku na kumuamrisha
baba yao atoke na fedha.
“Nilipoona
hivyo nilijaribu kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani, lakini mmoja
wa wauaji aliingia ndani na kunitoa nje ya nyumba yetu, huku akiniuliza
wakati wale vijana saba
wanachukuliwa na polisi mimi nilikuwa wapi.
“Waliendelea
kuniuliza kama nina habari ninayoijua, huku wakiwa wameshika mapanga na
bunduki, ndipo waliponiambia wapo kwa ajili ya kutetea dini yetu.
“Baadaye
waliniruhusu niingie ndani na kulala, lakini niliendelea kusikia
vishindo vya kipigo na watu wakikoroma ambayo ilikuwa ni ishara ya kuwa
baba yangu alikuwa anakata roho pamoja na watu wengine,” alisema.
Mtoto
mkubwa wa marehemu, Abuu Mkola, alisema vijana saba ambao sasa
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi awali walionekana katika Kitongoji cha
Kibatini wakiwa wanakimbia kusikojulikana.
Alisema
baada ya hali hiyo baba yake ambaye ni marehemu, Mkola Hussein
akishirikiana na wananchi wa mtaa huo walitoa taarifa kwa Jeshi la
Polisi ambao walikuja na kuwakamata vijana hao lakini mmoja wao
alifanikiwa kukimbia.
Abuu
alisema kuwa katika tukio la juzi, wauaji hao wakati wanamchukua baba
yake walisema wanawahitaji vijana wao saba waliokamatwa na polisi,
lakini aliposema hajui ndipo walimuunganisha na watu wengine kwa ajili
ya kumchinja.
Bunge Lataka Taarifa
Ofisi
ya Bunge imeiagiza Serikali kutoa taarifa rasmi kuhusu mauaji
yanayoendelea nchini ili kuwatoa hofu wananchi waliopo katika maeneo
mbalimbali.
Akitoa
maagizo hayo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alisema Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni anapaswa kuzungumza na
Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo yote ambayo yametokea mauaji
ili aweze kutoa taarifa ndani ya Bunge.
“Waziri
atuletee taarifa kwa sababu Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) yupo hapa na
waziri anayehusika na mambo ya Bunge yupo, naomba watuletee taarifa kwa
sababu mauaji yamekuwa yakitokea mara nyingi na tumekuwa tukiwasihi
Serikali ituletee taarifa na si mtakuwa mnazitafuta,” alisema Dk. Tulia.
Baada ya maelezo hayo Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisimama na kuomba mwongozo chini ya kanuni 68 (7).
“Mheshimiwa
Naibu Spika pamoja na haya uliyoyatolea maelezo juu ya mauaji
yanayotokea katika nchi yetu, nimelazimika kuomba mwongozo huu kwa
sababu matukio yaliyoanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali na maeneo
mengine mambo haya tuliwahi kuyauliza Serikali na kuahidi watayatolea
ufafanuzi.
“Sasa
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani amekwenda kuangalia na atazungumzia
jambo hilo wakati mambo haya wabunge tulishaiomba Serikali itoe
ufafanuzi ni jinsi gani inajipanga kukabiliana nayo,” alisema Lugola.
0 comments:
Post a Comment