Mwanafunzi
wa mwaka wa kwanza, Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM), Fredrick Joseph (25), ameuawa kwa kushambuliwa kwa kipigo
na watu wanaosadikiwa kuwa ni wanafunzi wenzake wakati akitoka klabu ya
pombe (Bar).
Tukio
hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la chuo hicho ambapo
mwanafunzi huyo alisikika akipiga kelele ndipo walinzi wakafika na
kumkuta akiwa anagalagala njiani.
Akizungumzia
tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, amesema
mwanafunzi huyo ambaye ametokea Musoma mkoani Mara alishambuliwa kwa
kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiofahamika.
Amebainisha
mwanafunzi huyo alikutwa majira ya saa 10 alfajiri katika eneo hilo la
chuo hicho huku akisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu
huyo alikuwa na ugomvi na watu hao katika klabu ya pombe ya Canival Pub
iliyopo chuoni hapo.
“Alipoondoka
kurudi bwenini akiwa njiani alishambuliwa na watu hao wasiofahamika na
kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake, kipigo kilichosababisha kifo
chake wakati alipokimbizwa kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya
Dodoma,” alisema Mambosasa
Amesema
mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali hiyo kwa uchunguzi
zaidi na hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.
Alipoulizwa
kuwa taarifa za mwanafunzi huyo kushambuliwa na wenzake, Mambosasa
alisema kwasababu inadaiwa haifahamiki upelelezi bado unaendelea.
“Kwa
sababu mwenye bar si yupo, kama kuna ugomvi ambao ulikuwa unaendelea
tutajua tu, nimemuelekeza OCD kufuatilia ni nani waliokuwa wanakunywa
kwenye hiyo bar chuoni, ni lazima tu watakuwa wanachuo ili tuwabaini,”
Kamanda huyo amesema ameelekeza uchunguzi wa kina ufanyike kama kulikuwa na ugomvi ndio hao hao walienda kumtegea njiani.
Chanzo cha habari ambacho hakikutaka kutaja jina lake kwa madai kuwa siyo msemaji wa polisi kimesema
kuwa marehemu Joseph alikuwa anakunywa pombe pamoja na marafiki zake
lakini baada ya kulewa walianza ugomvi ambao hata hivyo waliamuliwa.
“Baada
ya kuamuliwa ule ugomvi wa awali ndipo wenzake walipokwenda kumsubiria
kwa mbele kwenye kichaka ambapo walimvamia na kumshambulia na kumwacha
karibu ya kufa,” kilisema chanzo hicho.
Kiliongeza
kuwa, baada ya kumwacha hapo na kutoweka ndipo walinzi wa chuo hicho
waliokuwa doria walimuokota na kumfikisha kwenye kituo kidogo cha polisi
kilichopo Chimwaga ambapo alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Dodoma alipofariki wakati akipatiwa matibabu.
Chanzo hicho kimesema hakuna mtuhumiwa hata mmoja anayeshikiliwa na polisi kwa kuwa wote waliomshambulia walitoroka na hawajulikani walipo.
0 comments:
Post a Comment