SERIKALI na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wametakiwa kukaa chini kutafuta suluhu ya mvutano unaoendelea kuhusu operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) ili kuepusha vurugu kutokea nchini maandamano hayo yatakapofanyika.
Rai hiyo ilitolewa na Taasisi ya Maridhiano inayoundwa na viongozi mbalimbali wa dini jijini Dar es Salaam jana.
Lengo la taasisi hiyo ni kuishauri serikali na kutafuta suluhu na viongozi wa Chadema walioanzisha operesheni hiyo.
Katibu
Mkuu wa taasisi hiyo, Mchungaji Osward Mlay, alisema ili kuepuka
machafuko yanayoweza kutokea wakati wa kutekeleza operesheni hiyo
Septemba mosi, mwaka huu huku Jeshi la Polisi likisema litauvunja Ukuta ni vyema pande zote mbili zikajadiliana na kupata mwafaka.
"Hakuna
jambo lililoshindikana mezani. Sisi kama taasisi ya maridhiano,
tunaiomba serikali ikae mezani na viongozi wa Chadema ili kumaliza
tofauti," alisema.
Mchungaji
Mlay aliongeza kuwa sababu ya kuwashawishi Chadema na serikali kufanya
maridhiano ni kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha amani ya nchi inadumu
na kuondokana na dhana ya viongozi wa dini kutafuta usuluhishi pindi
machafuko yanapotokea.
Alisema
wana jukumu la kuwashauri viongozi wote wa serikali pale wanapohisi
kunaweza kutokea uvunjifu wa amani na kwamba hawako tayari kukaa kimya
pindi wanapoona ishara ya vitendo hivyo kama lilivyo lengo lao.
Mchungaji
Mlay pia aliitaka Chadema kusitisha maandamano waliyopanga kufanya na
badala yake wakae mezani kuona namna wanavyoweza kudai demokrasia kwa
amani badala kutumia njia ya maandamano.
Pia
alivishauri vyombo vya dola kuongoza nchi kwa mujibu wa sheria na
kanuni zinazosimamiwa na Katiba ya nchi bila kukandamiza demokrasia.
Alisema
wananchi pia wanapaswa kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani kama
kufanya maandamano yasiyo na tija kwa taifa ili kusitokee vurugu
zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Naye Sheikh Mohamed Hariri, alisema wanategemea serikali na Chadema watatafuta suluhu badala ya kusubiri machafuko yatokee.
0 comments:
Post a Comment