Hatimaye Jeshi la Polisi
limetoa kibali cha kufanya mkutano wa hadhara kwa Mbunge wa Iringa
Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, lakini limeweka mlolongo wa masharti
ambayo atalazimika kuyatii kuepuka rabsha.
Wakati Jeshi la Polisi
likitoa masharti hayo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema
vyama vya upinzani vitaendelea kuendesha mikutano ya hadhara licha ya
kufungua kesi Mahakama Kuu ya kupinga zuio la shughuli hizo, huku
akisema amri ya kuzuia wanasiasa kufanya mikutano nje ya maeneo yao
imetolewa bila ya kusoma sheria.
Mkoani Iringa, Jeshi la Polisi lilitoa masharti hayo baada ya Msigwa, ambaye anaongoza Jimbo la Iringa
Mjini kwa kipindi cha pili mfululizo, kutaarifu kuwa atafanya mkutano wa
hadhara kuanzia Septemba Mosi, siku ambayo Chadema imepanga kuanza
operesheni ya nchi nzima inayoiita “ya kupinga udiktekta Tanzania”.
Katika barua aliyomwandikia Mchungaji Msigwa juzi, Mkuu wa Polisi wa
Wilaya ya Iringa (OCD), Y. Z Mjengi amerejea barua ya mbunge huyo yenye
kumbukumbu namba MB/IR/M/05 ya Agosti Mosi mwaka huu, inayohusu mikutano
ya hadhara kuanzia Agosti 3 hadi 22, ikianza saa 8:00 mchana hadi 12:00
jioni.
Kupitia barua hiyo, ambayo Msigwa alithibitisha kuipokea, Jeshi
la Polisi limesema limeridhia kwa sababu lengo la mkutano wake ni
kuhamasisha maendeleo na kupokea kero za wananchi, kazi ambayo inatakiwa
kufanywa na mbunge wa eneo husika.
“Natarajia mkutano wako (Msigwa)
utakuwa wa amani na utulivu bila kumkashifu mtu wa chama kingine,”
anasema Mjengi katika barua hiyo.
“Mikutano yote hiyo kibali kimetolewa kwako kama mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini. Sitarajii
mtu mwingine kutoka nje ya Mkoa wa Iringa kuja kukusemea kuhusu
maendeleo ya jimbo lako au kuja kupokea kero za wananchi wako na
kuzijibia wakati hiyo ni kazi ya mwenye himaya ambaye ni wewe.
“Kashfa,
kejeli, matusi na maneno ya uchochezi kwa viongozi wa Serikali
vitahesabiwa ni uvunjifu wa amani na hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi yako na zitapelekea kuzuiliwa kufanya mikutano yako
inayoendelea.”
Barua hiyo inaishia kwa maneno yaliyoandikwa kwa herufi
kubwa. “Kumbuka: Amani ya Tanzania italindwa na kila Mtanzania kwa hiyo
ni jukumu lako wewe Mhe. Mbunge kutekeleza jukumu la ulinzi wa amani.
Kwa pamoja tutaweza,” inasema barua hiyo.
0 comments:
Post a Comment