Rais Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Taarifa ya Mwaka ya utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Kamishna Valentino Mlowola Ikulu jijini Dar es Salaam April 11,2016.Picha na Ikulu. **** Hussein Makame-Maelezo
Jumla
ya washitakiwa 572 wamepatikana na hatia kufuatia tuhuma za rushwa
zilizowakabili katika mahakama mbalimbali nchini katika kipindi cha
mwaka 2010 hadi 2015.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) Kamishna Valentino Mlowola katika taarifa iliyotolewa
kwa niaba yake na Afisa habari wa taasisi hiyo Mussa Misalaba.
Taarifa
hiyo inaonesha kuongezeka kwa idadi ya washitakiwa waliopatikana na
hatia ambapo mwaka 2010 washitakiwa 61 walitiwa hatiani wakati hadi
kufikia Desemba 2015 mahakama iliwatia hatiani washitakiwa 188.
Alisema
katika mwaka 2015 (Januari-Desemba) jumla ya matukio ya rushwa 5,000
yaliripotiwa na aina ya rushwa iliyoripotiwa mara nyingi ni matumizi
mabaya ya madaraka.
Taarifa
hiyo inaonesha kuwa katika kipindi hicho cha miaka 6 kuanzia mwaka 2010
hadi 2015, kesi mpya 1,691 zilizofikishwa mahakamani zikiwemo kesi 227
zilizofikishwa mwaka 2010, kesi 193 (2011), kesi 288 (2012), kesi 343
(2013), kesi 256 (2014) huku kesi 384 zikifikishwa mahakamani mwaka
2015.
Aliongeza
kuwa kesi zilizokuwa zinaendelea mahakamani kuanzia mwaka 2010 hadi
2015 zilikuwa 3,321 huku washitakiwa walioachiwa huru na mahakama katika
kipindi hicho wakiwa 646.
Kwa
upande wa kesi za rushwa zilizoondolewa mahakamani kutokana na sababu
mbalimbali kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 zilikuwa 162 kati ya hizo mwaka
2010 zilikuwa kesi 30, mwaka 2011 kesi 26 na mwaka 2012 kesi 24.
Kwa mwaka 2013 kulikuwa na kesi 17 zilizoondolewa mahakamani,wakati mwaka 2014 zilikuwa kesi 33 huku mwaka 2015 zikiwa kesi 32.
Mbali na kesi hizo, Kamishna Mlowola alisema kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 kesi 54 zilikatiwa.
Kamishna
Mlowola alimtaka kila mwananchi kutekeleza jukumu lake la kikatiba na
kisheria katika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.
Kifungu
cha 39 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka
2007 kinatamka kuwa “kila mtu anayefahamu kutendeka kwa kosa au
anafahamu kusudio la mtu mwingine kutenda kosa chini ya Sheria hii
anatakiwa kutoa taarifa TAKUKURU”.
“Hivyo,
tunamsihi kila Mtanzania asijiingize katika vitendo vya rushwa na
asinyamaze anapofahamu kutendeka kwa vitendo hivyo au hata kuwa na
wasiwasi na mali zinazomilikiwa na mtu yeyote.” Alisema.
Alifafanua
kuwa njia mojawapo nyepesi ya kuifikia TAKUKURU ni kupiga simu bure
kwenda namba 113 au *113# (USSD) na kutoa taarifa za rushwa kwa muda
wote wa saa 24.
Akizungumzia
jinsi ya kukabiliana na vitendo vya rushwa, Kamishna Mlowola alisema ni
wajibu kwa kila mwananchi kuzuia rushwa kwa kujijengea uelewa wa
taratibu za eneo analokwenda kupata huduma na kupambana na rushwa kwa
kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyotokea au vilivyotokea ili
hatua za kisheria zichukuliwe.
0 comments:
Post a Comment