Thursday 26 May 2016

#MICHEZO>>>>UWEPO GUARDIOLA, KLOPP, WENGER, MOURINHO, CONTE, NI KUREJEA KWA UBORA WA EPL ULAYA?.Fahamu zaidi hapa.

Na Mahmoud Rajab
Hatimaye Jose Mourinho anarudi tena kundini na kukutana na mahasimu wake wakubwa katika soka ambao ni Pep Guardiola, Wenger na Klopp (ambaye vilevile ana historia na Pep Guardiola pia) bila kusahau Conte ambaye ni moja ya makocha wenye ushawishi duniani.

Uwepo wa makocha hao itakuwa ni vita kubwa mithili ya vita vya ‘super-eagles’. Msimu ujao ama hakika utakuwa ni msimu utakaosheheni mchuano mkubwa wa makocha kwa makocha bila kusahau magoli hodari yatakayokuwa yakifungwa miongoni mwa timu hizo kutokana na ufundi wa makocha wanaozifundisha.

Ujio wa Jose Mourinho kama kocha wa Manchester United unabashiri upinzani mkubwa na usio na mfano ambao pengine haujawahi kutokea katika ligi nyingine. Maana upinzani huu utahusisha miongoni mwa makocha bora sita duniani.

‘Battle’ ya wanaume hao itakuwa ni Mourinho, Pep Guardiola atakayekuwa Manchester City, Arsene Wenger wa Arsenal, Jurgen Klopp wa Liverpool (kocha aliyejaa ari ya upambanaji na uhamasishaji), bila ya kusahau Muitaliano wa Chelsea Antonio Conte.

Tunataka kumsahau mtu ambaye atakuwa akipigana kulibakisha taji lake? hapana, huyu si mwingine bali ni ‘babu’ Claudio Ranieri.

Tafsiri ya upinzani huu itakuwa nini?, ikumbukwe tu hawa ni miongoni mwa makocha bora watano duniani ambao wanakutana kwenye ligi moja.

Kwa kipindi kirefu ligi ya England imekuwa dhaifu mbele ya ligi kama Uhispania na Ujerumani kutokana na timu zake kutofanya vizuri mbele ya timu za ligi hiyo.

Kwa miaka mitatu kama si minne mfululizo tumekuwa tukishuhudia timu kutoka Ujeruamani (hasa Bayern Munich) na Hispania (Barcelona, Real Madrid na Atletico Madrid) zikitinga hatua ya nusu fainali na fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hii inatokana na ubora, malengo na nia zilizopo ndani ya klabu hizo hasa kutokana na uwepo wa makocha wenye ushawishi kwa wachezaji bila kusahau ubora wa ligi ambao unatokana na ubora wa makocha na wachezaji kutokana uwekezaji mkubwa unaofanyika.

Pep Guardiola ni kocha mwenye mafanikio makubwa Ulaya, ameipa Barca UEFA mara mbili, akiwa na Bayern amefika nusu fainali mara zote kwa miaka yake mitatu amabyo amedumu pale.

Jurgen Klopp alifanya vizuri akiwa na Dortmund akiifikisha mpaka fainali ya UEFA mwaka 2013.
Vivyo hivyo Conte amefanya makubwa akiwa na Juventus, akiipa ndoo ya Serie A mfululizo. 

Historia ya Mourinho pia inajulikana bila kusahau Arsene Wenger.
Kuna upinzani mkubwa kati ya Jose na Pep, huu upinzani ulianza wakati wawili hao walipokutana wakati wa michuano ya ligi ya mabingwa mwaka 2008 Jose aliifunga Barcelona ya Pep na kuitupa nje hatua ya nusu fainali.

Miaka miwili baadaye Jose Mourinho anakuja kuwa kocha wa  Real Madrid na kuchagiza kwa kiasi kikubwa upinzani wao na kuwa mahasimu wakubwa katika maisha yao ya ukocha.
Jose v/s Arsene? Mourinho na Wenger ni mahasimu wakubwa sana na mara nyingi wamekuwa wakirushiana vijembe vya hapa na pale. Mourinho ameshawahi kumwita Wenger “mtaalamu wa kufeli (specialist in failure)”.

Itakuwa inatukumbusha namna ambavyo mwaka 2014 pale Mourinho na Wenger waliposhikana mashati kwenye eneo lao la kujidai (touch line). Sasa kurejea kwa Mourinho ni zaidi ya upinzani kwa Arsene Wenger.

Vipi Jose na Ranieri ambaye mara zote amekuwa ni mtu wa watu? Hapa hakutakuwa na tatizo licha ya wawili hao kukutana katika maeneo tofauti tofauti, kuanzai pale Italia wakati Mourinho alipokuwa Inter, wakati Ranieri akiwa Juventus na Roma.

Lakini ubingwa wa Leicester utakuwa ni chagizo la kuwepo kwa upinzani kati yao, kwani ikumbukwe kuwa wakati anawasili nchini England kuinoa Leicester, Mourinho alisema: “Wakati nikiwa Italy alikuwa moja ya wapinzani wangu, hivyo hatuwezi kuwa marafiki”, sasa kwanini Ranieri na Mourinho watakuwa ni mahasimu wakubwa msimu ujao? Ni kwasababu wakati Ranieri akitaka kuutetea ubingwa wake basi Mourinho atakuwa akijithidi kuuchukua hivyo kamwe hatawakuwa marafiki kwa saababu ni watu ambao watakuwa wakipigania taji moja.

Kuna vita kati ya Klopp na Guardiola–wameshawahi kukutana Ujerumani hawa wakati Klopp akiwa Dortmund Guardiola alikuwa Bayern. Walikuwa ni wapinzani wakubwa sana. Klopp tayari ameshamuonya mpinzani wake kwamba kamwe asitarajie kuja kuitawala ligi ya England kama alivyofanya wakati akiwa na Barcelona nchini Hispania na Bayern Munich nchini Ujerumani.

Kocha mpya wa Chelsea Antonio Conte yeye ni mtu wa kazi hana masihara hata kidogo, si mtu wa kuremba, ni mtu anayependa mfumo wa kazi tu “no-nonsense approach’.

Ugeni wake kwenye lugha ya Kiingereza unaweza kumfanya asikwaruzane na makocha wenzake lakini Andrea Prilo anasema: “Conte anapozungumza kukulenga wewe, basi maneno yake yanachoma na kuharibu kabisa akili yako, hii ni endapo utakuwa umemuudhi.” Sasa kwa hali hii tutegemee upinzani mkubwa kutokana na makocha wote kuwa na misimamo thabiti kwa kile wanachokiamini.

Ranieri anaweza kuwa na presha, kwanza kuwa kwenye Ligi ya Mabingwa na pili kutetea taji lake la EPL.

Huku Klopp naye anaweza kuwa nafaida kubwa kutokana na kikosi chake cha Liverpool kutokuwa kwenye michuano ya Ulaya na kupata muda mwingi wa kuweka presha kwenye ligi. Conte pengine anaweza kuhitaji muda kidogo ili kuijenga Chelsea ambayo imepotea katika msimu huu wa ligi uliomalizika.

Wenger naye ameahidi kuongeza nguvu kwenye kikosi chake ili kupambana kwa hali na mali kuwania ubingwa wa ligi kuu na Ligi ya Mabingwa baada ya msimu huu timu yake kumaliza katika nafasi ya pili.

Kwa kumalizia tu ni kwamba La Liga ina wachezaji bora, Serie A ina ubora aina fulani. Ujerumani ina ushindani kwa baadhi ya timu. Lakini msimu ujao wa EPL utakuwa ni wa kipekee kutokana kusheheni makocha wenye ushawishi ambao watasababisha ligi kuwa ngumu pengine kuliko miaka mingi iliyopita.

Hali hii itarudisha ushindani wa vilabu vya England kupigania taji la Ulaya kama ambavyo walikuwa wakifanya miaka ya nyuma kabla ya kupotea miaka ya hivi karibuni.

Tusubiri tuone je ujio wa Guardiola, Conte na Mourinho na uwepo wa Wenger na Klopp utarudisha hadhi ya vilabu vya England barani Ulaya baada kupoteza nguvu kwenye miaka ya hivi karibuni?
Matumaini yangu ni kwamba tutaanza kuona timu za England zikianza tena kufanya vizuri UEFA, kuingia nyingi kuanzia robo fainali, nusu fainali na ikiwezekana fainali.

0 comments:

Post a Comment