Friday 27 May 2016

#YALIYOJIRI>>>>Waziri Mbarawa Asema Wazee Hawatakiwi Tena katika Kampuni ya Simu ya TTCL.Fahamu zaidi hapa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema wakati umefika kwa wazee wanaofanya kazi katika Kampuni ya Simu ya TTCL, kuwaachia vijana kwa kuwa sekta ya mawasiliano hivi sasa ina ushindani mkubwa.

Akizindua nembo mpya ya kampuni hiyo na mtandao unaotumia teknolojia ya 4G LTE jana, Profesa Mbarawa alisema wazee wamekuwa watu wa kuzungumza zaidi ofisini, kuliko kufanya kazi na kubuni mbinu mpya zenye kuhimili ushindani.

Mbarawa alisema uzinduzi wa nembo mpya katika kampuni hiyo, hautakuwa na maana ikiwa wafanyakazi wa kampuni hiyo hawatabadilika na kutoa huduma zitakazowavutia wateja.

Aliishauri menejimenti kutoajiri watumishi kwa kujuana, bali watoe fursa kwa vijana wenye uwezo wa kuhimili ushindani unaotokana na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano.

Aidha, aliwataka vijana kutumia fursa hiyo kwa kuchapa kazi ili TTCL yenye sura mpya ifike mbali kimaendeleo na kuwa kati ya kampuni bora zaidi za mawasiliano nchini.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua thabiti za kuboresha na kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini na kusimamia vyema huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili zisaidie katika jitihada za nchi kujiletea maendeleo.

Alisema sekta ya habari na mawasiliano inagusa shughuli nyingi za maisha yetu ya kila siku, kijamii, kiuchumi na kimaendeleo na kuongeza kuwa hivi sasa huduma hizi sio tena jambo la ziada katika maisha ya kila siku bali ni huduma za msingi zenye kipaumbele cha juu katika maisha.

Akizungumzia maombi ya wananchi ya kutaka kusogezwa mbele kwa siku ya kuzima simu feki, waziri alisema Serikali haitasogeza mbele siku hiyo.

“Siku ya Juni 16, mwezi ujao Serikali itazima simu na vifaa vingine vya mawasiliano feki bila kuongeza muda, huu ni muda wa watu kujiandaa,” alisema.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni hiyo, Edwina Lupembe alisema TTCL wakati wowote kuanzia sasa itaanzisha huduma ya usafirishaji wa fedha kama zilivyo kampuni nyingine za mkononi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura alisema mabadiliko ya nembo hiyo yametokana na kampuni hiyo kuongeza huduma zinazotolewa kwa wateja.

0 comments:

Post a Comment