Katika
kesi hiyo ya uchochezi ambayo, mshitakiwa wa kwanza ni Jabir Idrissa
mwandishi mwandamizi wa gazeti la MAWIO huku Simon Mkina ambaye ni
mhariri wa gazeti hilo akiwa ni mshitakiwa wa pili.
Aidha
Ismail Mahboob, mchapishaji wa gazeti hilo ni mshitakiwa wa tatu na
Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) anayedaiwa kutoa
taarifa za uchochezi zilizochapwa na MAWIO akishitakiwa kama mshitakiwa
wa nne.
Akisoma
mashtaka hayo Paul Kadushi, Wakili wa Serikali Mbele ya Thomas Simba,
hakimu Mkazi mahakama ya Kisutu amesema watu hao wanashitakiwa kwa
makosa matano.
Shitaka
namba moja ni la kupanga njama za kutoa chapisho la uchochezi, kosa
linalodaiwa kutendwa kati ya tarehe 12 na 14 Januari mwaka huu ambapo;
Idrisa,
Mkina na Lissu katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam
walipanga njama za kuchapisha taarifa za uchochezi kinyume na sheria ya
magazeti kifungu cha 32(1)(a).
Shitaka
namba mbili linawakabili pia mwandishi Idrissa, mhariri Mkina na mbunge
Lissu, kwa kuandika habari za uchochezi zilizochapwa katika gazeti la
MAWIO toleo namba 182 yenye kichwa cha habari “Machafuko yaja Zanzibar.”
Shitaka
la tatu linamkabili mshitakiwa namba tatu Ismail Mehboob ambapo,
anatuhumiwa kuwa, 13 Januari katika jengo la Jamana, Ilala alichapisha
gazeti la MAWIO lenye habari ya uchochezi kinyume na sheria ya magazeti
kifungu cha 32 (1) (c).
Shitaka
la nne linamkabili pia mtuhumiwa namba tatu (Mehboob) kwa kuchapisha
gazeti hilo bila kuwasilisha hati ya kiapo kwa msajili wa magazeti
kinyume na sheria ya magazeti kifungu namba 6 na 12 (a).
Katika
kosa la tano, mshitakiwa namba moja (Idrissa), namba mbili (Mkina) na
namba nne (Lissu), wanatuhumiwa kuchochea hofu miongoni mwa wananchi kwa
kuchapisha habari “Machafuko yaja Zanzibar” na kwamba habari hiyo
ingeweza kuzua vita au umwagaji damu.
Baada
ya kusomewa mashtaka hayo mshitakiwa namba mbili (Mkina) na namba tatu
(Mehbooob) walikana mashitaka yao huku mshitakiwa Idrissa na Lissu
wakishindwa kufika mahakamani kutokana na sababu mbalimbali.
Hata
hivyo Peter Kibatala wakili wa washitakiwa ameiomba mahakama kuitupilia
mbali kesi hiyo kwa madai kuwa haina mashiko yoyote kisheria.
Kibatala
amefafanua kuwa, kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai
kifungu cha 89 (A) mtu hawezi kushitakiwa kwa kosa la uchochezi bila
idhini ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka ya serikali (DPP).
Huku
akiongeza kuwa kati ya mashitaka yote matano ambayo serikali
imeyawasilisha mahakamani ni shitaka moja tu (la tatu) ndilo lenye
idhini ya DPP na hivyo akaiomba mahakama kufuta shitaka namba moja,
mbili, nne na tano.
Wakili
huyo aliomba mahakama pia kulifuta shitaka la tatu kwani licha ya kuwa
na idhini ya DPP lakini linakosa mashiko kwasababu lipo nje ya wigo wa
kisheria uliowekwa na sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Kibatala
amesema sheria ya magazeti namba 4 ya mwaka 1976 kifungu cha 31(2)
a,b,c,d inafafanua kuwa, “Kitendo, maneno au chapisho halitakuwa la
uchochezi ikiwa litakuwa linaonesha mapungufu au makosa ya serikali na
kuitahadharisha ijisahihishe.”
Huku
akihitimisha hoja zake kwa kusema, mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu
haina uwezo wa kuisikiliza kesi hiyo kwa kuwa washitakiwa wanashitakiwa
kwa kosa la kuchochea uvunjifu wa amani visiwani Zanzibar.
“Sheria
ya magazeti ya 1976 siyo sheria ya Muungano, Zanzibar wanayo sheria yao
ya magazeti kwahiyo mahakama hii haiwezi kusikiliza mashitaka haya
kwasababu yanahusu uchochezi wa uvunjifu wa amani Zanzibar.”
Alihitimisha Kibatala.
Mawakili
wa upande wa serikali wakiongozwa na Paul Kadushi walipopewa nafasi ya
kujibu hoja zilizotolewa na wakili wa washitakiwa, waliiomba mahakama
kuwapa siku 14 ili kuweza kujipanga kujibu hoja hizo.
Ombi
lililokubaliwa na Hakimu Thomas Simba pamoja na wakili Kibatala na
hivyo kesi hiyo kuahirishwa mpaka 28 Juni 2016, saa tano kamili asubuhi
ambapo itatajwa tena.
0 comments:
Post a Comment