Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan leo
hii amezindua jukwaa la kuwezesha wanawake na akaunti maalum ya mikopo
ya MALAIKA inayolenga kuwawezesha wanawake wa hali ya chini kiuchumi
kupitia Benki ya wanawake katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar
es Salaam.
Akiongea
katika uzinduzi huo Mheshimiwa Samia Suluhu amesema kuwa lengo la
kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni kuwapa uwezo wanawake waweze kutoka katika
sekta isiyo rasmi na kuingia katika sekta rasmi na hivyo kuwainua
kiuchumi kwani mchango wa mwanamke mpaka sasa bado haujaongezeka
thamani.
Aidha
Bi Samia ameagiza kuwa kuanzia sasa asilimia 35% ya tenda za serikali
za mitaa ziende kwa wanawake na vijana ili kuwawezesha kiuchumi na
kuwataka wanawake kubadilika kifikra na hata wanapopata mikopo hii wawe
na nidhamu katika matumizi yake.
Hata
hivyo Mhe. Suluhu ametoa rai kwa mabenki kufikisha huduma zao vijijini
ili huduma ya mikopo iwafikie wanawake wachangie uchumi wa dunia na sio
tu kwa familia huku akiwahimiza wanawake kupendana,kushirikiana na
kusaidiana.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Watoto na
Wazee Dkt.Hamisi Kigwangala amesema kuwa serikali imeendelea kusaidia
wanawake katika Nyanja mbalimbali ikiwemo kuweka usawa wa jinsia kwa
wanawake kiuchumi ,kutoa vikwazo katika masoko na kuondoa mila
kandamizi.
Aidha
Dkt Kigwangala ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira
mazuri ya biashara kwa wanawake kwa kufanya mafunzo ya ujasiliamali na
kuweka sera nzuri ambayo yote haya yameainishwa katika ilani ya chama
cha mapinduzi ya 2015-2020 uku akieleza mafanikio makubwa ya benki ya
wanawake ambayo mpaka sasa imetoa mikopo yenye thamani ya bilioni 86.
Uzinduzi
wa Jukwaa hilo na akaunti ya MALAIKA ya mikopo uliendana na mada
mbalimbali kutoka kwa wadau mbalimbali kama Crdb,Benki ya wanawake,Nssf
,Wizara ya Viwanda na Biashara na Tcra.
0 comments:
Post a Comment