Ofisi
ya Spika imepokea taarifa ya kusudio la kuleta Bungeni Hoja ya
kumwondoa madarakani Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb) iliyowasilishwa na Mbunge wa
Simanjiro Mhe. Mhe. James Kinyasi Millya siku ya Jumatano tarehe 1 Juni,
2016.
Utaratibu
huo ni wa Kikatiba na upo chini ya Ibara ya 85(4) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ambapo pia umeainishwa katika
Kanuni ya 138 (1), ya kanuni za Kudumu za Bunge kuhusu utaratibu wa
Kumwondoa Naibu Spika Madarakani.
Baada
ya kupokea kusudio hilo, Kanuni za Bunge zinamtaka Spika kuiwasilisha
hoja hiyo katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili
ifanyiwe kazi.
Kutokana
na msingi huo wa kikanuni, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai (Mb)
anakusudia kuliwasilisha swala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge kama Kanuni inavyoelekeza ambapo kamati hiyo
itaangalia msingi wa hoja na endapo itaridhika, kanuni inaitaka Kamati
kuwasilisha hoja hiyo Bungeni ili ijadiliwe.
Aidha,
Kanuni ya 138 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inamtaka Spika kukalia
kiti wakati wa mjadala wa hoja ya kumwondoa Naibu Spika Madarakani.
Hivyo
basi, suala lililowasilishwa na Mhe. James Kinyasi Millya kuhusu
kusudio la kumwondoa Naibu Spika Madarakani, tayari limepokelewa na lipo
katika Ofisi ya Spika kwa ajili ya utekelezaji wa masharti ya Kanuni.
Imetolewa na,
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge
DODOMA
6 Juni, 2016.
0 comments:
Post a Comment