Sakata Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) limezidi kupanuka baada ya wanafunzi waliorudishwa nyumbani kupinga kuitwa vilaza.
Jana
wawakilishi wa wanafunzi hao ambao waliambatana na viongozi wa Mtandao
wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), walisema wanapinga pia hatua ya kutimuliwa
chuoni.
Akizungumza
kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Gibson Johnson alisema wanasikitika
kuona wanavyozushiwa tuhuma mbalimbali kuhusiana na wao kujiunga na chuo
hicho.
Alisema
wamekuwa wakijiuliza sababu za Serikali zinazotaka kuhalalisha
kutimuliwa kwao chuoni kuwa hawakuwa na sifa, jambo ambalo si la kweli.
“Siyo kweli kwamba sisi ni vilaza (wanafunzi wasiofanya vizuri darasani) na waliofeli na kupata daraja sifuri.
“Sisi
ni wanafunzi tuliofaulu kwa viwango vilivyohitajika kwa daraja la
kwanza hadi la tatu na tulipangiwa shule za kuendelea na masomo ya
kidato cha tano na sita, lakini tulibadili na kuamua kujiunga Udom,
hivyo tunaomba Serikali itumie busara zake.
“Hatuwezi kwenda kusoma kidato cha tano na sita kwa kuwa tumepoteza muda wetu.”
Alisema
wanamshauri Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako na Rais John
Magufuli kutumia busara kuwarudisha chuoni kumalizia masomo yao.
Katibu
Mkuu wa TSNP, Alphonce Lusako aliitaka Serikali ichukukue hatua kwa
waliohusika kudahili wanafunzi wasio na vigezo na kuwawajibisha.
“Lakini
pia wanafunzi wafidiwe fedha na muda waliopoteza kwa wakati wote
waliokuwa chuoni, kama hawatapewa haki zao, sisi tutashirikiana na wadau
wa elimu zikiwamo asasi za utetezi wa kisheria kutafuta haki mahakamani,” alisema Lusako.
Udom yazungumza
Ofisa
uhusiano wa Udom, Beatrice Baltazali alisema wanafunzi hao wote
walifaulu vizuri wakiwa na daraja la kwanza, pili na wachache daraja la
tatu.
“Wanafunzi
wote walikuwa na nafasi ya kwenda kidato cha tano, lakini kwa kuwa
waliahidiwa ajira, waliona wapitie huku kwa kuwa watapata ajira ya moja
kwa moja,” alisema.
Beatrice
alisema walimu wa Udom walikuwa wanalipwa fedha za ziada kuwafundisha
wanafunzi wa programu hiyo kwa kuwa walikuwa wanatumia muda mwingi zaidi
ya kiwango walichokuwa wamepangiwa.
“Kutokana
na madai ya malipo hayo, mkaguzi wa ndani aligundua kuna tatizo, ndiyo
walimu nao wakaamua kugoma, wanafunzi wakawa hawafundishwi Serikali
ikaamua warudishwe nyumbani,” alisema Beatrice.
0 comments:
Post a Comment