Saturday 29 August 2015

#YALIYOJIRI>>>Dr. Mwakyembe azungumzia Richmond kumuhusu Lowassa.

Mhe Mwakyembe amkaanga Lowassa kuhusu kadhia ya Richmond na kusema kuwa asikwepe maana tume ya Bunge ilimkuta na hatia na ikabidi ajiuzulu Uwaziri Mkuu.

Ameeleza hayo kwenye mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais kupitia CCM Mhe JPM leo huko Kyela katika mfululizo wa kampeni za mgombea huyo. Mhe Mwakyembe kaeleza kadhia hiyo kwa maelfu ya wananchi waliokuwa wakishangilia tangu mwanzo hadi mwisho na wameahidi na kuapa kutotoa kura zao kwa Lowassa!

Alieleza kuwa leo waTanzania wanalipia umeme kwa bei ya juu kutokana na uroho wa Fisadi huyo kwavile Tanesco iliingizwa kwenye mkataba mbovu na pia gharama za mabilioni zilizolipwa kufuatia mkataba mbovu na kesi zilizojiri baada ya mkataba kusitishwa!

Wakati huo huo aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe Mwakipesile, aliyestaafu ameuambia mkutano huo kuwa yeye hawezi kukihama chama cha Mapinduzi kilichomsomesha na kukulia kama mwanachama.

Hii inavunja uongo uliozushwa dhidi yake kuwa kakihama chama hicho na kuhamia UKAWA!
Mbeya. Mgombea ubunge jimbo la Kyela, Dk Harrison Mwakyembe amesema moto wa kashfa ya mkataba wa kufua umeme wa dharura na kampuni ya Richmond haujazimika, hivyo mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa anaweza kufunguliwa “kesi ya magendo”.

Dk Mwakyembe, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyochunguza sakata la kuipa kampuni hiyo ya Marekani zabuni ya kufua umeme wa dharura mwaka 2008, aliliambia Bunge wakati wa majumuisho ya mjadala kuwa kamati yake haikusoma taarifa kamili ya suala hilo kwa hofu kuwa Serikali nzima ingeondolewa na kuomba uchunguzi mpya ufanyike ili yaibuliwe mengi zaidi.

Lakini miaka saba baada ya kashfa hiyo kuisha kwa Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu, Dk Mwakyembe ambaye ni mwanasheria kitaaluma, ameliibua tena wakati wa kampeni za mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli mjini Kyela.

Akizungumza katika mkutano huo jana, Dk Mwakyembe alisema suala la Richmond lilikuwa limekwisha, lakini anaona kuna watu wanalifungua.

“Kwa sasa ninasubiri nione iwapo (kesho) leo wakati wa uzinduzi wa kampeni za Ukawa litagusiwa, nitaweka bayana mambo yote ambayo hayakuongewa bungeni kipindi kile,” alisema Dk Mwakyembe.

“Nimesikia mtu mmoja akisema ‘jamani kama mgombea wa urais wa Ukawa alikuwa na makosa mbona hamkupeleka mahakamani?’ Unajua wanasema elimu ndogo ni janga, naomba wote wanisikie mimi ni mwalimu wa sheria, kesi zote za jinai hazina ukomo, acha kuchezea moto kwenye petroli. Tunaweza kufungulia kesi ya magendo, “ alisema Dk Mwakyembe kwa ukali na akishangiliwa na wakazi wa Mbeya mjini.

“Chondechonde, atakayekuja kuwa rais (Magufuli) anachukia sana ufisadi na alishatangaza ataunda mahakama maalumu ya mafisadi. Chondechonde, tusiichezee Tanzania, naomba wana-Mbeya kura zote kwa Magufuli.”

Wanasheria walonga

Kauli hiyo ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeibua hisia tofauti kutoka kwa wanasheria, huku wakili wa kujitegemea, Semgalawe Charles akikubaliana na kutokuwapo kwa kikomo cha kesi za masuala hayo, lakini akasema Lowassa hakupatikana na hatia wakati ripoti ya Kamati ya Mwakyembe iliposomwa bungeni.

Alisema mahakama na vyombo vingine ndivyo vyenye mamlaka ya kutoa hukumu na endapo kungekuwa na hukumu Lowassa asingepata nafasi ya kugombea urais.

Maoni kama hayo yalitolewa na mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba ambaye alisema wakati ripoti ile ikisomwa, hakukuwa na hukumu badala yake Waziri Mkuu wa kipindi kile aliambiwa ajipime na kujitathmini.

Akizungumza jana, mwanasheria mwingine, Fulgence Masawe alisema tatizo watu wanashindwa kutofauti tuhuma za kisiasa na jinai za mahakama, Lowassa alikuwa na tuhuma za kisiasa na ndiyo maana alijiuzuru.

“Kama ingekuwa ni jinai angechukuliwa hatua mapema hata urais asingeweza kugombea,” alisema Masawe.

“Tatizo la nchi hii ni kutochukua maamuzi kwa wakati matatizo yake ndiyo haya. Wanakumbuka shuka kumeshakucha. Lowassa aliwajibika kisiasa siyo jinai. Kama jinai sidhani kama angepata fursa hii anayogombania hivi sasa,” alisema Masawe.

CHANZO: Lowassa kushtakiwa - Kitaifa | Mwananchi -
Lowassa kushtakiwa - Kitaifa | Mwananchi

0 comments:

Post a Comment