Friday 15 September 2017

Jeshi la Polisi Limeapiga Marufuku Maombi ya Kumuombea Tundu Lissu Yaliyopangwa Kufanyika Jumapili.

Kamishna Kanda maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambo Sasa amepiga marufuku maandamano na maombi yanayotaka kufanywa na CHADEMA siku ya Jumapili kumuombea Tundu Lissu kwenye uwanja wa TP Sinza Dar es Salaam na kusema hiyo siyo sehemu ya maombezi.

Lazaro Mambo Sasa amesema hayo leo wakati akifanya mahojiano na waandishi wa habari na kusema kuwa hawezi kuruhusu mkusanyiko wa watu na kuwataka watu ambao wanataka kumuombea Tundu Lissu kwenda kwenye nyumba za ibada na kumuombea lakini si kufanya mkusanyiko huo ambao wao CHADEMA wanataka kufanya.

"Hatutaruhusu mkusanyiko wowote usio na kibali, yapo maeneo ambayo kimsingi yanaendesha maombi hayo, yapo makanisa ipo misikiti na mahali pengine ambako pengine ni rasmi kwa shughuli hiyo, kupitia kwenu nasema hakutakuwa na kusanyiko hilo, yapo maneno ambayo yanaendelea kutolewa kupitia taarifa zao walizotoa ambayo maneno hayo kimsingi kila anayesikiliza anajua nia yao ni nini. Na sisi tukishaona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani hatuwezi kuhurusu mkusanyiko wa watu kwa hiyo mkusanyiko wa maombi hayo ni marufuku, tunaruhusu mwenye uwezo hata wa kukesha kanisani aende kwani ni mahali rasmi kwa maombi" alisisitiza Mambo Sasa

Aidha Kamanda Mambo Sasa ametolea ufafanuzi juu ya wanachama wa CUF ambao waliomba kufanya maandamano siku ya Jumapili Septemba 17, 2017 kwa ajili ya kuwapokea baadhi ya wabunge saba wa chama hicho ambao wameapishwa siku ya karibuni bungeni na kusema jambo hilo haliwezekani na yoyote ambaye atakiuka maagizo hayo basi ataishia mikononi mwa polisi.
"Sambamba na hilo naomba niseme kwa wale wanachama wa CUF ambao wameomba tarehe 17 kuwapokea wabunge wa CUF wanaotoka kuapishwa Dodoma walikuwa wameomba kufanya maandamano waanzie Kimara kuelekea Buguruni tumeshatoa maelekezo kuhusu hilo kuwa maandamano hayaruhusiwi na yoyote atakaye jaribu kufanya maandamano ataishia mikononi mwa polisi" alisema Kamanda Mambo Sasa

Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) leo asubuhi lilitoa taarifa kwa umma kuwa siku ya Jumapili litafanya maombezi ya kitaifa kwenye uwanja wa TP uliopo Sinza Darajani kumuombea Mbuge Tundu Lissu ambaye alishambuliwa na risasi na watu wasiojulikana ili aweze kupona kwa haraka na kurudi kuendelea na shughuli zake, jambo ambalo limepigwa na jeshi la polisi.

TOA MAONI YAKO

Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment