Alfajiri
 ya tarehe 7 Novemba 2016, tunaamka na kukutana na habari za kusikitisha
 kuwa Mzee Samwel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania ametangulia mbele ya haki. Babu alikuwa mgonjwa kwa
 kitambo kidogo akisumbuliwa na saratani ya tezi dume.
Majonzi ni makubwa kwa Taifa kutokana na sababu kubwa kwamba Samwel John Sitta alitumikia nchi yetu kwa muda mrefu na kwa uadilifu mkubwa.
Sisi
 wengine pia kwa kiasi fulani kukua kwetu kisiasa kumetokana na utumishi
 wake uliotukuka kwa nchi yetu alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania. Katika tanzia hii ninamkumbuka Mzee Sitta Kwa 
namna nilivyofahamiana naye binafsi na namna nilivyomshuhudia katika 
kazi zake.
Sitta
 ananigusa mimi binafsi moja kwa moja. Alikuwa babu yangu. Tukiwa 
bungeni akiniandikia kitu alikuwa akitumia neno hilo “babu” kwa mwandiko
 wake mzuri usiotoka kwenye kumbukumbu zangu kabisa.
Aliniapisha
 kiapo cha ubunge Desemba 29, 2005. Maneno ambayo aliniambia baada ya 
kunikabidhi Kanuni za Bunge na Katiba ya Nchi niliyaandika kwenye 
daftari langu la kumbukumbu siku hiyo hiyo jioni.
Baada
 ya kula kiapo cha utii na cha uaminifu kawaida wabunge hupewa mkono na 
mwapishaji na kupewa nyaraka za kazi. Kwa upande wangu Mzee Sitta 
alinikumbatia na kuniambia, “utakuwa kiongozi muhimu sana kwa nchi yetu.
 You have a bright future.”
Maneno
 haya hayajawahi kutoka katika kumbukumbu zangu na kila nikipata 
misukosuko yangu kisiasa huyakumbuka na wakati mwingine yeye mwenyewe 
alikuwa akinipigia na kunikumbusha na kunitia moyo. Babu alikuwa mlezi 
wa wanasiasa vijana.
Sitta
 pia amenilea kwa kunisomesha. Mwaka 1996 nilikuwa mwanafunzi wa Shule 
ya Sekondari ya Galanos jijini Tanga nikisomea mchepuo wa Historia, 
Jiografia na Uchumi (HGE).
Hali
 ya hewa ya Tanga haikunipenda, hivyo nikawa naumwaumwa sana. Pia 
nilitaka kusoma Hesabu badala ya Historia. Wakati wa likizo ya Desemba 
mwaka 1996, nilitoka Tanga nikaenda Dar es Salaam, Wizara ya Elimu 
kuomba uhamisho kwenda shule yenye Somo la Hesabu, kidato cha Tano na 
Sita. Nikakataliwa. Lakini nikaambiwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya 
Sekondari wakati huo Bwana Ndeki alisoma na Samwel Sitta.
Kipindi
 hicho Mzee Sitta akiwa Mkurugenzi wa Investments Promotion Centre (IPC)
 kabla haijabadilishwa jina kuwa Tanzania Investments Centre (TIC). 
Nikaenda Ofisi za IPC mahali ambapo leo ni CRDB Tawi la Azikiwe.
Nilipofika
 Katibu Muhtasi wake akaniuliza kama nina miadi na bosi wake, nikasema 
hapana. Akaniambia hawezi kukuona. Nikasisitiza sana na kumlilia dada 
yule aniruhusu dakika chache tu. Akaniruhusu.
Nilipofika
 Mzee Sitta aliniuliza shida zangu kwa heshima kubwa. Nikamwambia kwamba
 ninataka kuhama shule. Akaniomba matokeo yangu ya Kidato cha Nne, 
nikampa maana nilikuwa natembea nayo. Alipoyasoma akaniambia, “wewe 
hupaswi kuhangaika kutafuta shule maana kwa matokeo yako unaweza kusoma 
shule yoyote nchini ya chaguo lako”. Akainua simu akampigia Bwana Ndeki.
 Kisha akaniandikia kikaratasi niende wizarani muda uleule. Nilipofika 
wizarani nikapewa uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mazengo.
Nilipotoka
 nje ya wizara nikakutana na kijana mwingine anaomba uhamisho, yeye 
anatoka Mazengo anataka kwenda Tosamaganga, Iringa. Akaniambia, achana 
na Mazengo hakuna mwalimu wa Uchumi na hali ya vyoo ni mbaya sana. 
Nikarudi kwa Mkurugenzi. Mzee aliyenipa uhamisho aliponiona narudi na 
kumwambia sitaki Mazengo akachukua fomu zangu za uhamisho na akachukua 
‘whiteout’ akafuta Mazengo na kuweka Tosamaganga huku akisema kwa hasira
 “ nyie watoto wa wakubwa bwana”. Sikujali nikaenda zangu Tosamaganga 
kusoma Economics, Geography na Mathematics (EGM).
Sitta
 akaendelea kufuatilia maendeleo yangu shuleni na baadaye Chuo Kikuu cha
 Dar es Salaam na Taasisi ya InWent nchini Ujerumani.
Nilipotoka
 Ujerumani kusoma masomo ya Juu ya Biashara ya Kimataifa mwaka 2004 
ilipaswa niwe na mradi wa kitaaluma. Nikachagua kuunganisha kampuni za 
Kijerumani na Tanzania kwa kuandika mradi wa kuchukua wafanyabiashiara 
20 kutoka Tanzania na kuwaunganisha na wengine 20 kutoka nchi za Jumuiya
 ya Ulaya.
Ilibidi
 kupata Taasisi ya Tanzania kwa ajili mradi huo na Mzee Sitta akawa 
mstari wa mbele kuhakikisha mradi unafanikiwa na tukautekeleza kwa 
umakini kwa msaada wa ofisa wa TIC aitwaye Phina Lyimo.
Mwaka
 mmoja baadaye tukakutana na Mzee Sitta bungeni, yeye akiwa Mbunge wa 
Jimbo la Urambo Mashariki na mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma 
Kaskazini. Ulezi wake ukaendelea mpaka mauti yalipomkuta leo mapema 
asubuhi (jana). Nimempoteza babu mlezi.
Sitta
 alikuwa mwana mageuzi (reformer) na kupitia uanamageuzi wake alifanya 
mabadiliko makubwa sana katika uendeshaji wa shughuli za Bunge. Sisi 
tuliohudumu kwenye Bunge la Tisa, tukimwita Spika wa Viwango na Kasi, 
tuliona wenyewe juhudi zake za kuliweka Bunge katika nafasi yake ya 
Kikatiba. Licha ya kuhakikisha kuwa maslahi ya Wabunge yanalingana na 
hadhi ya Bunge, alihakikisha pia kuwa Bunge linaisimamia Serikali sawa 
sawa. Haikuwa kazi rahisi sana kwani kulikuwa na mvutano mkubwa sana 
kati ya Spika Sitta na Waziri Mkuu Edward Lowasa katika kuleta 
mabadiliko hayo.
Tulikuwa
 tunaambiwa kuwa mvutano huo ulitokana na tetesi kwamba Sitta ndiye 
alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na hivyo kuwa na msuguano na 
aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo. Si Sitta wala Lowasa ambaye 
alithibitisha ama kukanusha tetesi hizo. Sitta ametangulia mbele ya 
haki, labda Edward Lowasa ataweza kusemea hili siku za usoni.
Sitta
 alitumia fursa ya msuguano huo kufanya mabadiliko makubwa ya kanuni za 
Bunge na kutoa uhuru mpana wa mawazo ndani ya Bunge na kuhakikisha kuwa 
taarifa za Kamati za Bunge na hususani Kamati za Usimamizi wa Serikali 
zinasomwa na kujadiliwa ndani ya Bunge kwa mujibu wa Kanuni.
Wakati
 wa Bunge la Nane, Taarifa za CAG hazikuwahi kusomwa hata mara moja. Ni 
kutokana na mabadiliko haya ya kanuni ndipo Kamati ya Bunge ya Hesabu za
 Mashirika ya Umma (Poac ) ilianzishwa Machi, mwaka 2008.
Nilichaguliwa
 kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa kamati hiyo na kuingia kwenye Kamati ya 
Uongozi ya Bunge ambayo kipindi hicho tuliiona kama kamati ya wabunge 
wazee. Namna nilivyoingia kuwa Mwenyekiti wa Poac nayo ni hadithi 
nyingine ya namna ya malezi ya kiuongozi yaliyofanywa na Spika Sitta.
Sikuwa
 nimejaza fomu kuomba Kamati ya Poac. Wakati huo ulikuwa ni wakati wa 
vuguvugu la Buzwagi (Mkataba wa Madini uliosainiwa na Waziri wa Nishati 
hotelini nchini Uingereza kwa siri ). Nilikuwa mjini Bagamoyo kwenye 
kazi za Kamati ya Bomani nikiwa na Harrison Mwakyembe na Ezekiel Maige.
Spika
 wa Bunge akanipigia simu, akaniambia “Babu, kesho kuna uchaguzi wa 
Kamati za Bunge. Nimekuteua Kamati ya Poac ambayo ni kamati mpya 
itakayokuwa chini ya Kambi ya Upinzani. Najua hukuomba kuwa mjumbe wa 
kamati hii, lakini nahitaji damu changa kwenye Kamati ya Uongozi ya 
Bunge. Naomba unikubalie na kesho uwepo Dar es Salaam kwa ajili ya 
uchaguzi na ugombee. Utashinda maana nimeshafanya kazi yangu”. Sikuwa na
 namna ya kukataa japo nilitaka sana kuendelea kuwa Kamati ya Fedha na 
Uchumi chini ya Abdallah Kigoda, ama Kamati ya Nishati na Madini chini 
ya Mzee William Shelukindo.
Ombi
 la Mzee ni amri. Nikawa Mwenyektii wa Poac na kuwa mmoja wa washauri 
wakuu wa Spika wa Bunge. Kamati ya PAC ikawa chini ya Mzee John Cheyo na
 Kamati ya Laac ikawa chini ya Dk Wilibrod Slaa. Ilikuwa ni Bunge lenye 
meno kweli kweli.
Spika
 Sitta alikuwa mbabe. Ubabe wake ulimsababisha kufanya maamuzi ambayo 
wakati mwingine yalimweka kwenye matatizo na wananchi. Mfano mzuri ni 
suala la Hoja Binafsi ya Buzwagi na Hoja ya Wizi wa Fedha Benki Kuu ( 
Epa). Mwanzoni, Spika alikuwa upande wa wabunge wenye hoja hiyo yaani 
mimi na Dk Slaa kiasi cha kuziboresha hoja zile kwa kalamu yake 
mwenyewe. Wabunge wa chama chake hawakuwa wanapenda hoja hizi na hivyo 
Waziri Mkuu Lowasa akamweka kwenye wakati mgumu sana wa kuegemea upande 
wa Serikali. Hoja ya Dk Slaa akaitupa kuwa ‘ ni makaratasi ya 
kuokoteza’. Hoja yangu akaiingiza bungeni na akasimamia kusimamishwa 
kwangu bungeni. Wananchi walimkasirikia sana.
Siku
 moja usiku, nikiwa nyumbani kwa Freeman Mbowe Mikocheni, Sitta 
akanipigia simu kulalamika kuwa wafuasi wangu wanamtukana kwa meseji. 
Akaniambia niwakataze. Nilimkubalia tu, lakini sikuwa na uwezo huo. Nchi
 ilikuwa imevimba. Ilikuwa Oktoba 2007, Sitta alijua namna ya kusoma 
nchi na kuwapa watakacho, wakati mwingine. Mwezi Novemba, katika kujibu 
kiu ya wananchi kuhusu uwajibikaji na kufuta makosa ya Buzwagi na Epa, 
Spika alisimamia kuundwa kwa Kamati Teule kuchunguza suala la Mkataba wa
 Richmond. Yaliyofuata yalikuwa historia. Taarifa ya Kamati Teule 
ilisababisha ‘kuanguka’ kwa Serikali kwa mara ya kwanza katika hsitoria 
ya Tanzania, Waziri Mkuu Lowasa alilazimika kujiuzulu ndani ya Bunge, 
Baraza la Mawaziri likavunjika na Serikali mpya kuundwa chini ya Mizengo
 Kayanza Pinda.
Spika
 Samwel Sitta akawa ni Spika pekee wa nchi yetu aliyeshuhudia uundwaji 
wa Serikali mbili ndani ya miaka mitano ya uspika wake. Mzee Msekwa yeye
 alikaa miaka 10 na Waziri Mkuu mmoja, ingawa mwaka 1993-1995 naye 
aliona mabadiliko ya mawaziri wakuu, kutoka John Malecela kwenda kwa 
Cleopa Msuya. Baada ya kujiuzulu kwa Lowasa, Samwel Sitta hakurudi nyuma
 tena. Aliendelea kuwa Spika wa Viwango mpaka alipomaliza muda wake 
katika Bunge la Tisa.
Spika
 Sitta alikuwa mwepesi kuomba msamaha alipokosea. Nakumbuka siku moja 
mwaka 2009 alimfukuza bungeni mzee mwenzake John Cheyo kwa makosa ambayo
 Cheyo hakufanya. Baadhi yetu tukakasirishwa sana na kitendo kile. 
Nikaenda kumwona Mzee Sitta ofisini kumwuliza kulikoni amdhalilishe 
mwenzake namna ile. Akanieleza kuwa hakuwa sawa na atamwomba radhi John 
Cheyo. Tukiwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge kwa ajenda za kawaida 
tu, Mzee Sitta akamwomba radhi Mzee Cheyo.
Nikikumbuka
 kisa hiki nacheka sana maana Jaji Werema aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa 
Serikali alicheka mpaka kuanguka chini. Sababu? Mzee Sitta aliketi 
kwenye kiti chake, wenyeviti wote wa kamati tukiwa tumetulia tuanze 
kikao. Mzee Sitta akasema, “John, naomba radhi kwa tukio lililotokea 
bungeni wiki iliyopita. Sijui nilikuwa nina nini siku hiyo, nadhani 
nilisumbuliwa na watu wanaopitapita jimboni kutaka kunitoa, nisamehe 
mzee mwenzangu”. Kicheko ukumbi mzima na Cheyo akamkubalia radhi yake 
huku naye akicheka na yakaishia hapo. Wazee hawa wawili wameandika 
pamoja kitabu, ‘Bunge lenye Meno.’
Nimwelezeje
 zaidi Babu? Nimwelezeje zaidi Spika wa Kasi na Viwango Samwel Sitta? 
Mwanasiasa shupavu, jasiri, mwenye ngozi ngumu, mbabe, mnyeyekevu 
inapobidi na mwenye uthubutu. Tangulia Babu. Tangulia Mtemi wa 
Unyanyembe Samwel John Sitta. Umeondoka duniani lakini bado unaishi 
kupitia kazi zako kwa nchi yetu.
Mwandishi wa makala haya ni Kiongozi wa ACT- Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini.
 









 




 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
0 comments:
Post a Comment